Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Saturday, June 1, 2019

Serikali Yaja na Mfumo Mpya wa Ajira ‘Ajira Portal’ Kukabiliana na Vitendo vya Rushwa na Upendeleo

adv1
Na Mwandishi Wetu- MAELEZO, Dodoma
Serikali  imewataka Waajiri katika Utumishi wa Umma kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo mpya wa Maombi ya Kazi ‘ Ajira Portal’ uliopo chini ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira ili kuondoa changamoto zilizokuwepo awali kabla ya kujengwa kwa mfumo huo. 

Akizungumza wakati akifungua  mafunzo kwa waajiri leo Jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Kapteni (Mstaafu) George Mkuchika (Mb) amesema kuwa  Waajiri  wote watapaswa kutumia mfumo huo unaowashirikisha waajiri, muombaji wa ajira na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira. 

“ Hakuna sababu ya kila Taasisi kujenga mifumo ya kuendesha michakato ya ajira wakati tayari Serikali imeshawekeza katika ‘ Recruitment Portal’ kupitia Sekretarieti ya ajira” Alisistiza Mhe. Mkuchika 

Akifafanua amesema kuwa Serikali inahitaji watumishi wenye weledi unaoendana na mahitaji ya wakati hasa wakati huu Taifa linaposisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda. 

“Mfumo huu ni muarobaini dhidi ya vitendo vya rushwa,utashi  na upendeleo kwa kuwa utakuwa na uwezo wakuchagua waombaji wa ajira kulingana na sifa zao na nafasi walizoomba” Alisisitiza mhe. Mkuchika 

Aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika kutangaza nafasi za Ajira kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari . 

Pia alibainisha kuwa mchakato wa kuendesha zoezi zima la kutangaza nafasi za ajira hadi kukamilisha usaili litafanyika kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali na kuchelewesha upatikanaji wa majibu kwa waombaji wa nafasi za ajira. 

Aidha, alizitaka Taasisi zilizopo chini ya Msajili wa Hazina kutumia mfumo wa maombi ya kazi kuendesha michakato ya ajira ili kuwa na uhakika na takwimu sahihi, kumbukumbu na uhakika kwamba wanaoajiriwa Serikalini ni wale waliohakikiwa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) na Baraza la Mitihani (NECTA). 

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amesema kuwa mfumo huo una maeneo makuu matatu lakwanza likiwa ; Eneo la mwombaji wa kazi (Applicant), Eneo la Mwajiri (Employer), Eneo la Sekretarieti ya Ajira( Handling Interview Process and Placement/ Administrator). 

“ Mafunzo haya yamejikita kwenye eneo moja la Mwajiri (employer) ambao kwa mujibu wa mfumo wanajukumu kubwa kuandaa rasimu ya tangazo la ajira kwa mujibu wa muundo, kuingiza kibali cha ajira, kufuatilia maendeleo ya kibali husika na kupokea Watumishi wanaopangwa kwenye sehemu au Taasisi zao za Kazi” Alisisitiza  Bw. Daudi. 

Akizungumzia baadhi ya mafanikio ya Taasisi hiyo  Bw. Daudi amesema kuwa ni pamoja na kuokolewa kwa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali zilizokuwa zikitumika kwenye matangazo na pia kupunguza muda wa usaili na uendeshaji wa mchakato mzima wa maombi ya ajira. 

Pia kuongezeka kwa maombi ya kazi, kuongeza uwazi na pia mifumo ya TEHAMA imerahisisha utunzaji wa Taarifa na nyaraka mbalimbali za waombaji kazi. 

Mafunzo haya yaliyotolewa kwa siku mbili kuhusiana na mifumo ya Ajira licha ya kurahisisha utendaji kazi wa ofisi moja moja, pia yataondoa urasimu wa upatikanaji wa taarifa na yatawezesha taarifa kupatikana kwa wakati.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )