Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Thursday, June 14, 2018

Waganga Wakuu Waagizwa Kukagua Watoto Wachanga Kubaini Ukeketaji

Na Jacquiline Mrisho 
SERIKALI imewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha wanawafanyia uchunguzi watoto wachanga wanaopelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kubaini kama wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji.

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Arusha na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoazimishwa kitaifa jijini humo katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid Karume.

Dkt. Ndugulile amesema kutokana na watoto kuendelea kujengewa uwezo kuhusu hasara za ukeketaji wamekuwa wanajitahidi kutoa taarifa  sehemu husika hivyo wazazi wameamua kuanzisha mbinu mpya za kuwakeketa watoto wachanga jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

“Suala la ukeketaji watoto wachanga liko ndani ya uwezo wangu hivyo naagiza kutolewa kwa waraka kwa Waganga Wakuu wote nchini  kuwakagua watoto wanaoenda kliniki ili kubaini kama wamekeketwa na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi waliohusika na vitendo hivyo,” alisema Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa ukeketaji bado ni changamoto kubwa nchini ambapo takwimu za mwaka 2015 zimeonyesha bado kuna mikoa mitano ambayo iko juu ya wastani wa kitaifa katika suala la ukeketaji hivyo ni lazima agizo hilo litekelezwe kwa haraka ili kukomesha tatizo hilo.

Ameitaja mikoa inayoongoza kwa ukeketaji kuwa ni Mkoa wa Manyara unaongoza kwa asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha asilimia 41, Mara asilimia 32 na Singida asilimia 31.

Vile vile Dkt. Ndugulile ameelezea kukithiri kwa mimba za utotoni ambapo Mkoa wa Katavi unaongoza kwa asilimia 45, Tabora asilimia 43, Mara asilimia 37 na Shinyanga asilimia 34.

Ametoa rai kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanasambazwa katika ngazi zote nchini ili watoto wapate uwakilishi mkubwa wa masuala mbalimbali yanayowahusu.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Plan International, Benatus Sambili amesema kuwa shirika hilo linafanya kazi pamoja na Serikali katika kuziba mianya iliyopo katika jamii ambayo inazuia watoto kupata haki zao zikiwemo za kuwapa elimu na stadi za maisha pamoja na elimu ya kujitambua.

“Shirika letu lina miradi ambayo inawasaidia watoto ikiwemo miradi ya kupinga ndoa za utotoni katika mikoa ya Mara, Morogoro, Geita na Rukwa lenye lengo la kuwafikia zaidi ya watoto 28,755, mradi wa kuzuia ukatili wa kijinsia mashuleni ambapo tumelenga kuwafikia watoto 35,000 pamoja na mradi wa kupunguza na kuondoa ajira za watoto katika maeneo ya migodi kwa watoto zaidi ya 22,000” alisema Sambili .

Maadhimisho hayo hufanyika kila Juni 16 ambapo kwa mwaka huu yameadhimishwa Juni 13 kwa sababu siku husika itakuwa na muingiliano wa ratiba zingine, kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘kuelekea uchumi wa viwanda, tusiwaache watoto nyuma’.

 Watoto wa Mkoa wa Arusha wakiwa katika Maaandamano ya Siku ya myoto wa Afrika yenye Kauli Mbiu isemayo Kuelekea uchumi wa Viwanda Tusimuache Mtoto Nyuma.

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na watoto waliokusanyika katika kiwanja cha mpira cha Shkeih Amri Abed Jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.

Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Sihaba Nkinga akielezea chimbuko la Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Jijini Arusha.
chn
ap
Loading...
taboola dsk
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )