Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Friday, October 5, 2018

Ujenzi wa Terminal 3 Katika Uwanja wa Ndege JNIA Kugharimu Bilioni 560.....Utakuwa na Uwezo wa Kupokea Ndege 19 kubwa na Ndogo 11 Kwa Mpigo

juu
Jumanne wiki hii, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, alifanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo na hatua iliyofikiwa katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Uwanja huo una historia ndefu. Ulianzia katika kipindi kirefu miaka 62 iliyopita katika zama kabla ya uhuru wa Tanganyika, ikiitwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Baadaye lilijengwa jengo jipya la kisasa zaidi, ambalo baadaye likaitwa ‘Terminal Two’ wastani wa miongo mitatu na nusu iliyopita, kazi iliyoendana na upanuzi wa njia na mahitaji mengine ya uwanjani, kukidhi maboresho ya vigezo vya kimataifa nchini.

Baadaye, ikiwa ni kutambua mchango wa Rais wa Kwanza, Hayati Julius Nyerere, mageuzi na maboresho ya uwanja huo yanayoendelea kulingana na kukua mahitaji ya wateja wake, uwanja huo ulipewa jina lake.

Hivi sasa kuna mwendelezo wa awamu nyingine, sasa kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja huo unaoelekea ukingoni kwa miaka mitano hivi sasa na kuongeza kipande kingine cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘Terminal Three.’

Ujenzi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 560, ulianza mwezi Juni mwaka 2013 na unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Mei na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 82.

Akizungumza uwanjani hapo, Mwambe anaeleza kuwa uwanja huo utatokea fursa za uwekezaji, ikiwamo kujitokeza kwa kampuni mpya za ndege kuanza kutua Tanzania.

“Kampuni za ndege zikiongezeka maana yake kutakuwa na ushindani kwenye soko, hivyo itasaidia kupunguza gharama za usafiri wa ndege kwa wananchi. Ushindani huu ukiwapo maana yake abiria atachagua asafiri na aina ya shirika la ndege,” anaeleza.

Mwonekano wa uwanja huo mpya unabebwa na jengo lenye ghorofa tatu, ambayo ya kwanza itatumika kwa ajili ya wasafiri wanaofika, ghorofa ya pili ni kwa wasafiri wanaoondoka na ya tatu ni kwa ajili ya masuala ya utawala.

Mwambe anasema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo, utasaidia kuongeza tija kwenye uwekezaji, ambayo ni eneo analolisimamia kupitia TIC.

“Ni ukweli usiopingika kwamba, duniani nchi zenye miundombinu bora kama viwanja vya ndege vya kimataifa, barabara, bandari ndizo zinazopata wawekezaji wengi.

“Tumeshuhudia kupitia serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, maeneo haya niliyotaja amekuwa akiyapa kipaumbele ili kuhakikisha Tanzania ijayo inakuwa yenye uwekezaji mkubwa,” anasema.

Mwambe anasema, wiki iliyopita Watanzania walishuhudia Rais Dk. Magufuli alipozindua Barabara ya Juu ya Mfugale, iliyopo katika makutano ya Barabara ya Julius Nyerere kutoka Uwanja wa Ndege kuelekea mjini na ile ya Mandela, kutoka Ubungo kwenda Bandarini.

Pia, Mwambe anafafanua kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) unaendelea na taratibu za kuanza kwa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme nchini ‘Stiegler's Gorge’ zinaendelea.

“Kwetu TIC maboresho haya ni faraja, kwani yatachagiza uwepo wa mazingira bora ya biashara na uwekezaji na kuwezesha kuunga mkono juhudi zetu za kuvutia na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nchini,” anaeleza.

Mwambe anataja maeneo mengine ya uwekezaji ya wawekezaji wazawa wanakoshauriwa kuyachangamkia ni ya uendeshaji wa biashara ya magari madogo, maegesho, maduka, hoteli na maduka ya mvinyo.

Anasema matarajio ya serikali kwenye uwekezaji huo, ni kuhakikisha unatoa huduma nzuri kwa wadau wakiwamo watalii, wafanyabiashara na wawekezaji.

“Kuhakikisha unavutia zaidi wawekezaji, inatengeneza ajira kwa Watanzania, kodi inakusanywa kwa ajili ya kuendesha huduma za jamii na kuinua hali ya Watanzania na uchumi wa taifa,” anasema na kuongeza:

Mwambe anaishukuru serikali kujikita katika kuboresha na kuimarisha miundombinu ambayo itakayoleta mapinduzi ya ukuaji uchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TAA), Richard Mayongela, anasema kuwa uwanja huo utakapokamilika, utaondoa msongamano wa abiria wanaotumia sehemu ya ‘Terminal Two.’

“Terminal Two ilijengwa miaka 34 iliyopita, kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri zilizokuwa zikitolewa na ‘Terminal One’ iliyojengwa mwaka 1956 na ilikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 tu kwa mwaka,” anasema.

Anabainisha kuwa ‘Terminal Two’ ilijengwa kuwahudumia abiria milioni moja na nusu, lakini kwa sasa inahudumia hadi milioni 2.5 kwa mwaka.

“Idadi hii ni kubwa na imetokana na ongezeko la abiria na shughuli nyingine za usafirishaji, jambo ambalo linasababisha changamoto katika sekta ya anga kubaki palepale, ikiwamo kukosa ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wadau na mahitaji yao kwa ujumla,” anasema.

Mayongela anafafanua kwamba, kuna dira ya kukamilika upanuzi huo wa uwanja kutaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo nchini katika sekta ya anga na kutaongeza safari za ndege nyingi, kutua Tanzania.

“Mashirika ya ndege duniani yakiongezeka hapa, kutaongeza mapato kwa serikali na vilevile kutawezesha kuitangaza Tanzania kimataifa,” anasema na kuongeza:

“Ujenzi wa uwanja huu, ni mkombozi mkubwa wa Watanzania katika kuboresha sekta ya anga. Uwanja wa ndege tunaoutumia sasa, ulijengwa mwaka 1984. Hivyo, ni miaka 34 iliyopita,” anasema.

Anafafanua zaidi: “Kwa hiyo, utaona ni jinsi gani tunatoa huduma za usafiri wa anga kwa sasa, kwa miundombinu iliyokuwa imelenga kuhudumia abiria wachache wa kipindi cha miaka ya 1980.”

Kama alivyo bosi wa TIC, Mayongela anaishukuru serikali kwa maamuzi ya kuupanua uwanja huo, kwani umefanyika kwa wakati muafaka ukiendana na ukuaji uchumi na maendeleo ya nchi.

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa ‘Terminal Three’ itakapokamilika, itaruhusu ndege kubwa (Dream liner 8) kupakia na kushusha abiria na mizigo yao kwa wakati mmoja, wakati huo huo ndege tatu zikiwa kwenye eneo la maegesho.

“Kwa namna upanuzi huu ulivyofanyika, utawezesha kuhudumia ndege kubwa za kawaida zipatazo 19 na ndege ndogo 11 zinazoingia na kutoka nchini kwa wakati mmoja,” anasema.

Ziara hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, imefanyika kutokana na kituo hicho cha uwekezaji kuwa mdau mkubwa wa uwekezaji, pia kubadilishana mawazo, uzoefu na kushauriana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, kuhusu uwanja huo wa ndege.

Mayongela anasema, lengo lao ni kuhakikisha uwekezaji huo unavutia na kuchochea wawekezaji kuja zaidi Tanzania na kuirudishia faida serikali, Watanzania na taifa kwa jumla.

chn
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )