Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Monday, January 28, 2019

Waziri wa Mifugo Awabana Wawekezaji Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU)

juu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ametoa mwezi mmoja kwa wawekezaji walioingia mikataba ya uwekezaji kwenye Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kulipa deni la shilingi milioni 331.2 wanalodaiwa vinginevyo Serikali itavunja mikataba na wahusika wote watakamatwa na kutaifishwa mali zao.

Waziri Mpina ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza katika ziara ya kutembelea Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kwenye Visiwa vya Mbudya na Bongoyo ambapo ilibainika kuwa baadhi ya wawekezaji waliopewa maeneo kwenye hifadhi hizo kushindwa kuyaendeleza kwa mujibu wa mikataba sambamba na kushindwa kulipa tozo stahili za Serikali zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema Serikali haiwezi kukubali kuchezewa na wawekezaji ambao hawajajipanga na kuchelewesha uendelezaji wa fukwe na maeneo mengine ya urithi wa nchi yetu sambamba na kukwamisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Waziri Mpina alisema Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu ina utajiri na urithi mkubwa wa Tanzania kwa kuwa na fukwe ndefu na nzuri za kipekee duniani, makaburi yenye historia ya kuvutia, mazalia ya samaki, matumbawe yenye mvuto wa kipekee na ndege wa aina za kipekee ambao hawapatikani maeneo mengine duniani.

Mpina alisema pamoja na kuwapo vivutio hivyo vya kipekee, bado kitengo hicho hakijaweza kuvitangaza vivutio hivyo kikamilifu ambapo hadi sasa hakuna mabango kwenye malango ya kuingia nchini ikiwamo viwanja vya ndege, bandarini na mipakani na mikoani, hakuna matangazo kwenye vyombo vya habari, hivyo kuchangia wananchi kutofahamu urithi huo na kuwapo kwa idadi ndogo ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea hifadhi hizo.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza kuandaliwa mkakati wa kutangaza vivutio hivyo ili viweze kujulikana, idadi ya watalii kuongezeka pamoja na kukuza mapato ya Serikali, huku akisisitiza kuwa mkakati huo uwasilishwe wizarani kwake Februari 28, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, alionesha kushangazwa na taasisi hiyo kushindwa kujiendesha na kuendelea kutegemea ruzuku ya Serikali licha ya kuwapo fursa nyingi na vyanzo vingi vya mapato, hivyo alitoa mwezi mmoja kuandaliwa mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuifanya taasisi hiyo kujitegemea kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2019/2020.

Kuhusu kile kinachodaiwa kuwapo baadhi ya viongozi kuingilia na kuhujumu majukumu ya kitengo hicho kwa kuwaeleza uongo wananchi, Mpina amewataka watumishi wa taasisi hiyo kushikilia msimamo wa Sheria iliyoanzisha taasisi na kwamba kama kuna maelezo na mawazo ya kisera basi malalamiko hayo yawasilishwe kwa viongozi wakuu wa wizara.

Aidha, aliwahimiza watendaji wa kitengo hicho kubuni miradi mingine ya kiuchumi hasa katika maeneo ambayo zamani yalikuwa yakitumika kwa shughuli za uvuvi ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kujiongezea kipato na kuona thamani ya uwapo wa hifadhi hizo.

Pia aliagiza kufanyike tathmini ya ubora wa miundombinu na vifaa muhimu katika shughuli ya uhifadhi ili kuboresha utendaji kazi wa kitengo hicho. Vile vile ameagiza kuandaliwa kwa mpango biashara utakaowezesha kitengo kujiendesha kibiashara zaidi.

Kwa upande wake Meneja wa MPRU, John Komakoma, alimhakikishia Waziri kuwa maagizo yote aliyoyatoa atayasimamia kikamilifu kuona yanatekelezwa kwa wakati ili kuiwesha taasisi hiyo kutoa mchango unaostahili kwa pato la Taifa.

Komakoma alisema ili kuleta ufanisi wa kazi kitengo hicho kiko kwenye hatua ya mwisho ya mapitio ya Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Namba 29 ya mwaka 1994 ili kuiwezesha taasisi hiyo kuhifadhi maeneo tengefu yaliyoko kwenye mito mikubwa, mabwawa na maziwa kote nchini .

Pia alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 kitengo hicho kimepokea watalii 45,000 ambapo kati ya hao 26,000 ni watalii wa ndani 19,000 ni wa nje na kuingiza kiasi cha wastani wa shilingi bilioni 1.6 kwa mwaka ambapo idadi ya watalii na mapato yanatarajia kuongezeka katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

chn
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )