Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Tuesday, March 12, 2019

Mpina Azindua Mpango wa Kuendeleza Mifugo Nchini

juu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amezindua Mpango Kambambe wa Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini (Tanzania Livestock Master Plan-TLMP) huku akimtaka Katibu Mkuu Mifugo kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati huo ndani ya siku 30 ili utekelezaji uanze mara moja.

Akizindua mpango huo jijini Dar es Salaam, Waziri Mpina alisema, ni lazima mpango mkakati wa utekelezaji uwasilishwe ofisini kwake ndani ya kipindi hicho ili kuondoa dhana iliyojengeka ya mipango mingi kuandaliwa kwa muda mrefu na gharama kubwa, lakini usimamizi na utekelezaji wake kuwa dhaifu na kushindwa kuleta matokeo yaliyotarajiwa.

Alisema Tanzania ina mifugo mingi, ikiwa na asilimia 1.4 ya ng'ombe duniani na asilimia 11 ya ng'ombe Bara la Afrika wako Tanzania huku ikiwa ya pili barani Afrika baada ya Ethiopia.

Waziri Mpina alisema fursa na changamoto zimefanikisha kuandaliwa kwa mpango huo ili kuondoa vikwazo na kuweka mazingira wezeshi ya ufugaji, biashara na uwekezaji.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa malisho na maji, wafugaji kufukuzwa kila mahali, ukosefu wa dawa na chanjo za mifugo, ongezeko la bidhaa za mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi, uwekezaji wa kusuasua, ukosefu wa bei nzuri, soko la uhakika na mitaji na ukosefu wa mifugo iliyoboreshwa na huduma za utafiti.

Aliwataka wadau wa maendeleo waliofadhili mpango huo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) na Taasisi ya Bill & Melinda Gate Foundation, kutoishia kufadhili uandaaji wa mpango huo badala yake washiriki moja kwa moja kwenye utekelezaji wake.

Pia aliwataka watendaji wote wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa kujipanga na kushiriki katika utekelezaji wa mpango huo ili kuleta matokeo ya haraka.

Waziri Mpina pia aliitaka sekta binafsi, wafugaji, jumuiya za wafugaji, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za fedha kila mmoja kwa nafasi yake ashiriki kutekeleza mpango huo.

Kufuatia mpango huo, serikali italazimika kufanya marekebisho ya sera na sheria pamoja na kuanzisha mikakati na miongozo mipya ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo kwa ufanisi mkubwa.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema kuzinduliwa kwa mpango huo kumeiwezesha wizara yake kupanga matumizi bora ya ardhi ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.

"Ardhi yangu haina maana kama haitumiki vizuri, mimi nafurahi sasa mmejipanga na mmetengeneza mpango mzuri ambao utasaidia hata kunipa kazi ya kupanga matumizi ya kufanikisha mpango wenu, nataka nikuhakikishie mheshimiwa Mpina tuko pamoja najua mahitaji yenu,” alisema Lukuvi.

Katibu Mkuu Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema mpango huo ulianza kuandaliwa miaka mingi iliyopita, lakini sasa umekamilika na kuzinduliwa huku akimhakikishia Waziri Mpina kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wake ili kuleta matokeo ya haraka yanayotakiwa na Watanzania.
chn
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )