Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Sunday, March 3, 2019

Serikali Yataja Sababu za kusimamisha leseni ya Gazeti la The Citizen

juu
Serikali  imefafanua sababu na hatua ilizochukua kabla ya kusimamisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la The Citizen kwa siku saba huku ikishangaa wanaodai kuwa limefungiwa kutokana na kuikosoa serikali.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas ameainisha maonyo mbalimbali ambayo serikali iliwahi kuyatoa kwa gazeti hilo kabla ya adhabu hiyo ya kusimamishwa leseni iliyotolewa kuanzia Februari 27.

Mkurugenzi huyo wa Maelezo alisema alifanya uamuzi kutokana na mamlaka aliyopewa na kifungu cha 9 (b) ya Sheria Namba 12 ya Huduma ya vyombo vya Habari ya mwaka 2016.

“Uamuzi wa kusimamisha leseni kwa muda unatokana na gazeti hili kuchapisha habari mbalimbali za upotoshaji na za upande mmoja ambazo zinakiuka maadili na masharti ya leseni,” alisema Dk Abbas.

Alisema Februari 23 gazeti hilo kwa makusudi lilitoa taarifa za upotoshaji kwamba shilingi ya taifa inashuka ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

Habari hiyo ilinukuu wasemaji katika maduka ya kubadilisha fedha bila kutaja majina yao na pia ilinukuu wachumi bila kuwasiliana na Benki Kuu (BoT) yenye mamlaka ya kusimamia viwango vya ubadilishaji fedha.

Kuhusu madai kwamba gazeti hilo limefungiwa kutokana na kuikosoa serikali, alikanusha na kusema ukosoaji unaruhusiwa serikali inapokwenda kinyume na sera au utekelezaji wa jambo lolote.

Ametoa mfano, Februari 19 mwaka huu, serikali ililifutia leseni gazeti la ‘Tunatekeleza’ kwa kwenda kinyume na taaluma.

Amesema serikali ilichukua hatua licha ya kwamba gazeti hilo limekuwa likiandika habari chanya kuhusu serikali na lilikuwa likiunga mkono uongozi wa Rais John Magufuli.

“Gazeti lilikuwa likiandika habari chanya tu kuhusu serikali na lilikuwa likiunga mkono uongozi wa Rais Magufuli lakini lilichukuliwa hatua kulinda weledi,” alisema na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ustawi wa vyombo vya habari vinavyozingatia maadili.

Kwa mujibu wa Dk Abbas, gazeti la Citizen lilipewa haki ya kusikilizwa kama inavyoainishwa katika kanuni ya 27 (1) (a) ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2017.

Wahariri walipewa siku tatu za kujieleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka misingi ya uandishi wa habari na sheria.

Amesema wahariri wa gazeti hilo walijibu kwa maandishi wakiomba msamaha.

Amesema wasingeridhishwa na uamuzi, wangefuata utaratibu wa kisheria wa kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya habari kama ambavyo sheria inasema.

Sheria namba 12 ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 inatoa fursa kwa mtu ambaye chombo chake kimesimamishwa, chini ya kifungu cha 10 (1), kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ya habari endapo hakuridhishwa na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO.

Dk Abbas alianisha habari tofauti za upotoshaji zilizowahi kuchapishwa na gazeti hilo miongoni mwake ikiwa ni iliyochapishwa Julai 22 mwaka jana yenye kichwa cha habari “US Senator Raises Alarm on Tanzania” ikimnukuu seneta wa Marekani aliyeshutumu masuala ya haki za binadamu na demokrasia nchini.

Alisema mwandishi hakuzingatia misingi ya uandishi ya kuweka mizania kwa kutoa nafasi kwa mamlaka zinazohusika kujibu shutuma za seneta huyo. Serikali iliandikia gazeti barua ikilitaka kuzingatia maadili ya uandishi na likaahidi kujirekebisha.

Dk Abbas amesema pia Desemba mwaka jana, gazeti lilichapisha habari ambayo haikuwa na mizania iliyoonesha kwamba, Marekani imeitaja Tanzania katika orodha ya nchi ambazo raia wake wanaarifiwa kuchukua hadhari za kiusalama kutokana na matukio ya ugaidi.

“Siku chache baadaye, ubalozi wa Marekani hapa nchini ulilalamika habari hiyo na kuelezea kuwa tahadhari hiyo ilitolewa siku nyingi kinyume na habari husika. Gazeti liliomba msamaha kwa kuchapisha taarifa za uongo,” amesema.

Amesema vyombo vya habari vinavyoandika uchochezi vitaendelea kudhibitiwa ili kuhakikisha umma unapata haki ya habari zilizo sahihi.

Serikali imesajili magazeti na majarida 200, vituo vya redio 160 na vituo vya televisheni 40 hatua inayofanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoshika nafasi ya juu ya kuwa na vyombo vingi vya habari. Vipo pia vyombo vilivyojisajili mtandaoni.

Credit: Habarileo
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )