Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Saturday, July 20, 2019

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Hali Ya Uzalishaji Wa Mazao Ya Chakula Kwa Msimu Wa 2018/2019 Na Upatikanaji Wake Kwa Mwaka 2019/2020

juu
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2018/2019 na upatikanaji wake kwa mwaka 2019/2020
Ndugu Wanahabari, 
Kila mwaka kati ya mwezi mei na juni, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali hufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa chakula na upatikanaji ili kujua;
     i.        Hali ya kiujumla ya uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa chakula kwa Mikoa na Halmashauri zote
    ii.        Uzalishaji wa mazao ya chakula na utekelezaji wa malengo ya uzalishaji hadi tarehe 31 Mei kila mwaka.
  iii.        Athari za visumbufu katika uzalishaji wa mazao
  iv.        Bei ya mazao ya chakula na hali ya upatikanaji wa chakula sokoni katika Halmashauri zote na kuainisha maeneo yenye dalili ya uhaba
   v.        Hali ya unyeshaji wa mvua na mwenendo wa uzalishaji wa mazao mashambani
Ndugu Wanahabari
hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2013/2014 hadi 2017/2018 ambapo kwa msimu wa 2018/2019 nchi imejitosheleza ikilinganishwa na mahitaji.
Ndugu Wanahabari, 
katika kufanya tathmini ya hali ya chakula, hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wa chakula tunaangalia baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi kama vile mahindi, mtama na ulezi, mchele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi.
Ndugu Wanahabari, 
katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125 na imekuwa ikizalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,322,689. Mafanikio hayo yanatokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa nzuri, pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali pamoja na Wadau wengine wa masuala ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.
Ndugu Wanahabari, 
Wizara ya Kilimo mwezi Mei hadi Juni 2019 ilifanya Tathmini ya Hali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula kwa msimu wa 2018/2019 na Upatikanaji wa Chakula kwa  mwaka 2019/2020 katika mikoa yote 26 Tanzania Bara kwa lengo kubaini uzalishaji na mahitaji.
Ndugu Wanahabari, 
Matokeo yanaonesha kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/2019 utafikia tani 16,408,309 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain Equivalent) ambapo nafaka ni tani 9,007,909 na siyo nafaka tani 7,400,400.
Ndugu Wanahabari, 
Ikilinganishwa na msimu uliopita, uzalishaji wa mazao ya chakula umeshuka kwa tani 483,665 ambapo nafaka hususan mahindi yameshuka kwa tani 455,642 na mchele kwa tani 210,454. Aidha, uzalishaji wa siyonafaka (non cereals) umeongezeka kwa tani 46,283.
Ndugu Wanahabari, 
uzalishaji wa mazao ya nafaka ulifikia asilimia 103 na mazao yasiyo ya nafaka yalifikia asilimia 145. Hivyo, uzalishaji wa jumla wa mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia asilimi 119.
Ndugu Wanahabari, 
Aidha mchango wa uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/2019 unaonesha kuwa mahindi yamechangia kwa asilimia 35, muhogo kwa asilimia 17, mchele kwa asilimia 12, viazi kwa asilimia 10 na mazao mengine.
Ndugu Wanahabari, 
Pamoja na hali hiyo, utengamano wa usalama wa chakula unatarajiwa kuwa wa viwango tofauti kimkoa. Aidha, hali ya uwepo na upatikanaji wa chakula kwa sasa ni nzuri kutokana na uzalishaji mzuri wa msimu wa 2017/2018.
Ndugu Wanahabari
Kwa kuzingatia Kigezo cha Upimaji wa Kiwango cha Utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), matokeo yanaonesha kuwa kwa mwaka wa chakula 2019/2020, nchi itakuwa na kiwango cha Utoshelevu cha asilimia 119.
Ndugu Wanahabari
Tathmini imeonesha, hali ya chakula inatarajiwa kuwa ya kiwango cha Ziada kwenye mikoa 11 ya Rukwa, Ruvuma, Songwe, Katavi, Njombe, Mbeya, Kigoma, Iringa, Kagera, Morogoro, na Mtwara kwa asilimia 128 hadi 227. Aidha, kutakuwa na hali ya Utoshelevu  kwenye mikoa 7 ya Geita, Simiyu, Pwani, Lindi, Manyara, Singida na Tanga kwa asilimia 109 hadi 119 na Upungufu kwenye mikoa 8 ya Dodoma, Mara, Mwanza, Arusha, Tabora, Shinyanga na Kilimanjaro kwa asilimia kati ya  98 hadi 99.
Ndugu Wanahabari
Mkoa Dar es Salaam si miongoni mwa mikoa ya uzalishaji wa mazao na hivyo kujitosheleza kwa asilimia 3 tu kutokana na eneo dogo linalolimwa lisilokidhi mahitaji ya chakula ya wakaazi wake. Ingawa mkoa huu unawekwa kwenye upungufu wa chakula kwa maana ya uzalishaji katika mashamba, mkoa huu una vyakula vingi vinavyoingia sokoni kutoka katika mikoa 25 ya Tanzania bara na hivyo kuwa na Utoshelevu kwa vipindi vyote.  
Ndugu Wanahabari
Tathmini imebainisha kuwa uwepo wa maeneo (pockets) yenye dalili za upungufu wa chakula kwenye Halmashauri 46 katika mikoa 13 kama ifuatavyo;
·      Mkoa wa Dodoma katika Halmashauri 7 za Bahi, Chamwino, Chemba, Kondoa, Kongwa na Mpwapwa;
·   Mkoa wa Mara katika Halmashauri 5 za Bunda DC, Bunda TC, Musoma DC, Musoma MC na Rorya;
·     Mkoa wa Tabora katika Halmashauri 5 za Uyuyi, Igunga, Nzega DC, Nzega TC na Kaliua;
·   Mkoa wa Shinyanga katika Halmashauri 4 za Kishapu, Shinyanga DC, Shinyanga MC na Msalala;
·     Mkoa wa Kilimanjaro katika Halmashauri 4 za Mwanga, Same, Siha na Hai,
·  Mkoa wa Mwaza katika Halmashauri 4 za Misungwi, Ukerewe, Kwimba na Sengerema;
·       Mkoa wa Manyara katika Halmashauri 4 za Simanjiro, Kiteto, Hanang na Mbulu TC;
·        Mkoa wa Simiyu katika Halamshauri 4 za Itilima, Maswa, Meatu na Busega;
·        Mkoa wa Arusha katika Halamshauri 3 za Longido, Ngorongoro na Monduli;
·        Mkoa wa Singida katika Halmashauri 3 za Ikungi, Manyoni na Singida DC;
·        Mkoa wa Tanga katika Halmshauri 1 ya Tanga jiji;
·        Mkoa wa Lindi katika Halmashauri 1 ya Lindi DC na
·        Mkoa wa Iringa katika Halmashauri 1 ya Iringa DC.
Ndugu Wanahabari
Msimu wa uzalishaji wa 2018/2019 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali katika baadhi ya maeneo zilizoathiri uzalishaji wa mazao kwa viwango tofauti na kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa mazao hususan zao la mahindi. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-
(i)          Katika maeneo yanayopata mvua misimu miwili (Bimodal Areas) mvua za vuli katika maeneo mengi hazikufanya vizuri. Aidha, mvua za masika zilichelewa sana kuanza na hivyo kuathiri shughuli za kilimo katika maeneo hayo,
(ii)         Kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha kwenye baadhi ya maeneo ya nchi yanayopata mvua msimu mmoja (Unimodal Areas) hususan katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro, Mwanza, Mara, Simiyu na Manyara,
(iii)       Visumbufu hususan viwavijeshi vamizi (Fall Army Worm - FAW), panya na Kweleakwelea.
Ndugu Wanahabari
Kufuatia matokeo ya Tathmini hii, Serikali inachukua / itachukua hatua zifuatazo;
·        Kuimarisha Mfumo wa ukusanyaji taarifa za usalama wa chakula nchini ili kuweza kuchukua hatua stahiki pindi inapobidi,
·        Kufanya Tathmini ya Kina ya Hali ya Chakula na Lishe mapema katika Halmashauri zilizobainika kuwa na maeneo yenye viashiria vinavyoweza kusababisha upungufu wa chakula,
·        Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wanatarajia kuanza ununuzi wa mazao ya chakula kutoka kwenye maeneo yenye ziada,
·        Kuimarisha mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo viuatilifu, mbegu na mbolea.
·        TRA pamoja na Wataalam wa kilimo katika vituo vya mipaka ya nchi  kusimamia kikamilifu usafirishaji wa mazao yanayokwenda nje ya nchi ili kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za kiasi kinachosafirishwa nje ya nchi.
Ndugu Wanahabari
Niwatake wananchi wote nchini kuzalisha mazao ya chakula kwa kuzingatia kanda za kiekolojia, kuwa na hulka ya kuhifadhi chakula kulingana na mahitaji ya kaya pamoja  kutumia  mazao ya chakula kilichopatikana vizuri kiweze kutumika hadi kufikia msimu mwingine wa uzalishaji.
Aidha, Wakulima waliopata chakula cha ziada wanashauriwa  wasiharakishe kuuza mazao yao mapema bali wasubiri hadi bei zitakapokuwa nzuri ndipo wauze na kwa wale wenye waliopata utoshelevu kidogo wa chakula watumie vizuri mazao hayo kwa ajili ya chakula na si vinginevyo.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA 
Japhet Ngailonga Hasunga (Mb)
WAZIRI WA KILIMO
18 Julai 2019
ap
Loading...
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )