Wakufunzi wa mafunzo ya Kilimo nchini wameagizwa kufanya kazi
kwa weledi kwa lengo la kuwafundisha
wanafunzi kuelewa na kuwa mahili katika kilimo kibiashara.
Agizo hilo limetolewa leo Jijini Mbeya na Katibu Mkuu Wizara
ya Kilimo Gerald Kusaya alipotembelea na kuzungumza na watumishi na wanafunzi
wa chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MATI) Uyole.
Kusaya amevitaka vyuo vyote 14 vinavyotoa mafunzo ya Kilimo
vya umma na vile 15 vya binafsi kuhakikisha vinawafundisha wanafunzi taaluma ya
kufanya Kilimo biashara ili wakihitimu waweze kujiajili na kusaidia wakulima
kuzalisha mazao kwa faida
“ Hiki ni chuo cha kilimo lazima tuwafundishe vizuri
wanafunzi wetu ili wakitoka hapa wawe wanajua kila kitu katika sekta ya mazao
,hivyo wakufunzi wapeni nafasi wanafunzi wajifunze zaidi kwa vitendo na kutumia
teknolojia rahisi” alisisitiza Katibu Mkuu huyo
Aliongeza kusema vyuo vyote hasa vya umma vianzishe shughuli
na miradi ya kujiongezea kipato kwa kutumia ardhi na miundombinu iliyopo na
kupunguza utegemezi wa bajeti ya serikali.
Katika kufikia malengo hayo ya kufundisha Kilimo cha
kibiashara ,Katibu Mkuu huyo ameahidi kukichangia chuo cha MATI Uyole shilingi
milioni 30 ili kiongezee katika bajeti yake kununua trekta kwa ajili ya kazi za
uzalishaji mazao.
Pia amesema
atakisaidia chuo hicho pikipiki tatu kwa ajili ya wakufunzi, kompyuta tano na
vifaa vya TEHAMA ili chuo kianzishe maktaba mtandao (e-learning) pamoja na
kuwapatia wanafunzi magunia 20 ya mpunga ili wale.
Pia ameahidi kukipatia chuo cha MATI Uyole kitalu nyumba (
Green House) kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuzalisha mboga mboga
na matunda (horticulture.
Katika kukifanya chuo
hicho kinaongeza uzalishaji ameagiza uongozi wa chuo kuwasiliana na Tume ya Taifa
ya Umwagiliaji kwa ajili kuanzisha miundombinu ya umwagiliaji ili kuwasaidia
wanafunzi kujifunza vema kabla ya kuhitimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha MATI Uyole Emanuel Mwalukasa
alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa jitihada ambazo serikali kupitia wizara ya
Kilimo inafanya kuboresha mazingira ya ufundishaji.
Aidha Katibu Mkuu huyo alitembelea Kituo cha Utafiti wa
Kilimo (TARI) Uyole ambapo amewapongeza kwa kazi nzuri ya utafiti wa aina
nyingi bora za mbegu zenye matokeo mazuri kwa wakulima
Ameitaka taasisi hiyo kuongeza jitihada katika kufanya tafiti
zenye lengo la kusaidia wakulima kuzalisha mazao mengi kibiashara na kuchangia
katika uchumi wa taifa .
“Ninyi TARI mna deni kubwa kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli
kufanya utafiti katika Kilimo kionekane chenye tija na kukifanya cha kibiashara
na kuwezesha matokeo ya tafiti hizi za mbegu kuwafikia wakulima na maafisa
ugani vijijini” alisema Kusaya
Kuhusu maonesho ya Nanenane ameagiza taasisi zote za mafunzo
ya Kilimo na utafiti siku zote kuwezesha wakulima na wananchi kujifunza kilimo
na teknolojia muda wote ,hivyo elimu itolewe kwa watu wengi zaidi nchini ili
kuleta mapinduzi ya kilimo.
Akiwa mkoani Mbeya Katibu Mkuu Kusaya amekagua maandalizi ya
maonesho ya Nane nane katika viwanja vya John Mwakangale na kuwataka wadau
wajitokeze na kuendelea na maandalizi
Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya
Kilimo,Uvuvi na Mifugo Chagua Viongozi Bora 2020” ambapo kitaifa maonesho hayo
yatafanyika mkoani Simiyu .
Katibu Mkuu Kusaya yupo mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi
kutembelea taasisi zilizochini ya wizara yake na kuongea na watumishi ikiwa na
lengo la kuongeza tija katika utendaji kazi wenye matokeo chanya kwa sekta ya
Kilimo.
Imetolewa na ;
Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MBEYA
17.07.2020
Loading...
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi
==>>... << BOFYA HAPA Kui Install>>
Mgid
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )