Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Thursday, May 20, 2021

Waziri Mchengerwa Awataka Maafisa Wa Takukuru Kutunza Siri Za Wanaotoa Taarifa Za Vitendo Vya Rushwa


Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) kutotoa siri za wananchi wanaowasilisha taarifa za uwepo wa vitendo vya rushwa kwenye taasisi hiyo ili ziweze kufanyiwa kazi.

Akizungumza wakati wa kikao kazi chake na Viongozi wa TAKUKURU jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi (CP) Salum Hamduni kuhakikisha vyanzo vya taarifa za rushwa vinalindwa ili kuhamashisha wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazoiwezesha Serikali kulinda rasilimali za taifa.

Mhe. Mchengerwa amehimiza uadilifu kwa Watumishi wa TAKUKURU hususan kwenye eneo la utunzaji siri za watoa taarifa ili kuwajengea wananchi imani ya kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Utoaji wa siri za wanaowasilisha taarifa za vitendo vya rushwa, unahatarisha usalama wao, hivyo Mkurugenzi Mkuu uanze na suala hili ili tubaini watumishi wote wanaotoa siri za watoa taarifa na kuwachukulia hatua za kinidhamu.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewaasa watumishi hao kutenda haki wanaposhughulikia vitendo vya rushwa ili kutoitia dosari Ofisi hiyo inayoaminiwa na wananchi.

Kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais juu ya taasisi hiyo kujikita moja kwa moja katika majukumu yake, Mhe. Mchengerwa amewakumbusha Viongozi hao kutekeleza maelekezo hayo ipasavyo kwa kushughulikia masuala yanayohusiana na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi na si vinginevyo.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali ina imani na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni na Naibu wake Bi. Neema Mwakalyelye na ndio maana Mhe. Rais amewapa dhamana ya kuiongoza taasisi hiyo nyeti.

Akizungumza na viongozi wa TAKUKURU kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza watendaji wa TAKUKURU kutofanya kazi zisizoihusu TAKUKURU kama ambavyo Mhe. Rais na Waziri Mchengerwa wamekuwa wasisitiza.

Mhe. Ndejembi ameitaka TAKUKURU kuhakikisha inayakamilisha kwa wakati mashauri ya msingi yanayoihusu taasisi hiyo na kwa yale yasiyokuwa na msingi yafutwe ili kutoa fursa kwa taasisi hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yenye tija kwa taifa.

Kwa upande wake. Mkurugenzi wa TAKUKURU, CP Salum Hamduni amekiri kupokea maelekezo ya Mhe. Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi ndani ya muda aliolekeza.

Ili kutekeleza maelekezo ya Mhe. Mchengerwa kwa wakati, CP Hamduni amewataka watumishi wake kujitoa kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU ili kufikia malengo ya taasisi hiyo.

Mhe. Mchengerwa amefanya kikao kazi na Viongozi wa TAKUKURU mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo na Naibu wake kuapishwa na Mhe. Rais-Ikulu Jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuhimiza uwajibikaji na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi hiyo.

Tangazo
ap
Loading...
taboola dsk
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )

End: