Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Thursday, January 6, 2022

Mwinyi awafunda mabalozi wapya diplomasia ya uchumi


Rais  wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza haja kwa mabalozi wanaoiwakilisha nchi nje walioteuliwa hivi karibuni, kuipa kipaumbele sera ya diplomasia ya uchumi katika nchi wanazokwenda kufanya kazi.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana, Ikulu Zanzibar, alipokutana na kufanya mazungumzo na mabalozi hao.

Baadhi ya mabalozi hao na nchi wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania ni Perera Ame Silima (Visiwa vya Comoro), Said Shaib Mussa (Kuwait), Fredrick Kibuta (Urusi), Prof. Adelardus Kilangi (Brazil), Alex Kalua (Israel) na Said Mshana Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza mabalozi hao kwamba sera ya diplomasia ya uchumi ndiyo iliyopewa kipaumbele hivi sasa katika Tanzania, hivyo ni vyema wakaenda kuifanyia kazi ili uchumi wa Tanzania uzidi kuimarika.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaeleza mabalozi hao namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha uchumi wake ambao dira ni uchumi wa buluu.

Alisema utalii ni miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele kupitia uchumi huo wa buluu na kuwasisitiza mabalozi hao kuhakikisha wanaitumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar kiutalii katika nchi wanazokwenda.

Pia alisema mbali na utalii, ni vyema kuitangaza Zanzibar katika sekta za uchumi wa buluu zikiwamo uvuvi, mafuta na gesi asilia, uvuvi, kilimo cha mwani na bandari huku akisisitiza kwamba iwapo bahari itatumiwa vizuri maendeleo makubwa yatapatikana.

Dk. Mwinyi alisema Dira ya Uchumi wa Buluu inaweza kufanya kazi kwa nchi zote wanazokwenda kuiwakilisha Tanzania, hivyo akasisitiza haja ya kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo kadhaa ya viwanda nchini.

Sambamba na hayo, Dk. Miwnyi alisisitiza kwamba kwa upande wa Comoro ni vyema hatua za kurejesha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara ukafufuliwa kati ya nchi hiyo na Zanzibar.

Pia alieleza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Brazil hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta ya teknolojia, hivyo ni vyema wakawakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kuwekeza nchini badala ya kuagiza bidhaa kadhaa kutoka nchini humo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano ili kuimarisha sekta ya biashara na Kuwait sambamba na kutafuta namna ya kupeleka bidhaa mbalimbali nchini humo zinazotoka Tanzania.

Dk. Mwinyi alisema Urusi ni mdau mkubwa wa utalii nchini hivyo, ni vyema juhudi za makusudi zikaendelezwa kuhakikisha watalii wanakuja nchini sambamba na kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo ya utalii.

Awali, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ukiongozwa na Mwakilishi Mkaazi, Christine Musisi.

Katika mazungumzo hayo UNDP imekubali kutuma timu ya wataalamu ili kushirikiana na wataalamu walioko serikalini, ikiwa ni hatua ya kupata njia bora ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo kupitia sekta mbalimbali, ikiwamo uchumi wa buluu, kwa lengo la kupata mafanikio.


Tangazo
ap
Loading...
taboola dsk
ad

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )

End: