Asilimia 97 ya watoto
wanaozaliwa hunyonyeshwa maziwa ya mama, ikiwa asilimia 92 ya watoto
hunyonyeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhe.
Mwanaidi Khamis wakati akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu
kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama
kwa watoto kitaifa yanayofanyika kwenye halmashauri ya Ikungi Mkoani
Singida.
Mhe. Mwanaidi ameendelea kusema
kuwa 43% tu ya watoto ndio hunyonyeshwa hadi kipindi cha miaka miwili
na kuendelea huku takwimu zikionesha 57% tu ya watoto ndiyo hunyonyeshwa
maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chakula kingine wala maji
ndani ya kipindi cha miezi 6.
“Tafiti zinaeleza kuwa mtoto
akizaliwa na kuanza kunyonyeshwa maziwa ya mama ndani ya saa moja
kunaweza kuokoa uhai wake kwani kuchelewa kumnyonyesha mtoto kuna
changia kwa kiwango kikubwa vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28.”
Aliongeza.
Aidha, amesema hapa nchini
unyonyeshaji wa watoto wachanga ndani ya saa moja umefikia 90% hivi sasa
ikilinganishwa na 54% iliyokuwa mwaka 2018 wakati utoaji wa Vitamini A
kwa watoto wa miezi 6-59 nao umeongezeka kutoka 64% mwaka 2018 hadi
kufikia 97% hivi sasa.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo
aliwahimiza wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoa
huduma kwa wakati husika na kuwaasa wazazi kuendelea kuhudhuria Kliniki
kama inavyoagizwa pia wazazi kuwanyonyesha watoto wachanga maziwa ya
mama pekee kwa kipindi cha miezi sita bila kumlisha chakula kingine wala
maji pamoja na kuwanyonyesha watoto kwa kipindi cha miaka miwili na
zaidi.
“Kunyonyesha maziwa ya mama kuna
faida nyingi kwa mama na mtoto kwa kuwa kunaimarisha afya na ustawi wa
mama na mtoto, vilevile unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia aina
zote za utapiamlo kwa vile kuna kuwa na uhakika wa chakula kwa watoto
wachanga na wadogo”. Alisisitiza
Vile vile amesema ili kuimarisha
na kuendeleza juhudi za kulinda Afya ya watoto kupitia unyonyeshaji
maziwa ya mama, Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria,
kanuni na miongozo iliyopo juu ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama,
kuendelea kutenga fedha za kutekeleza afua za kuboresha ulishaji wa
watoto ikiwemo elimu ya Afya, lishe na huduma za msingi kwa wanawake
wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na kutoa miongozo na taarifa sahihi
kuhusu unyonyeshaji na namna ya kujikinga na magonjwa hasa ya mlipuko.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi
Mhe. Jerry Muro amewataka wakurugenzi na watoa huduma ya Afya wa
halmashauri yake kuendelea kutoa elimu juu ya unyonyeshaji na kuwasihi
wananchi kuepukana na mimba za utotoni.
“Changamoto zinazopelekea wazazi
kutonyonyesha watoto zao ni pamoja na mimba za utotoni kwakuwa hawajui
umuhimu wa kunyonyesha na wengine kuwa bize na kazi na hivyo kuacha
kunyonyesha watoto zao.” Amesema DC Muro
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya
ametoa rai kwa Serikali kuongeza muda wa ruhusa kwa wazazi wanaofanya
kazi ili kupata muda mwingi wa kuwanyonyesha watoto zao.
Maadhimisho hayo ya wiki ya
unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto kitaifa yanayofanyika kwenye
halmashauri ya Ikungi Mkoani Singida kuanzia 1-7 Augusti 2022 yenye
kauli mbiu isemayo CHUKUA HATUA ENDELEZA UNYONYESHAJI: ELIMISHA NA TOA
MSAADA
Loading...
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi
==>>... << BOFYA HAPA Kui Install>>
Mgid
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )