Friday, April 18, 2014

Taarifa ya jeshi la Polisi kuelekea sikukuu ya pasaka.....


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini katika suala la usalama wa maisha na mali zao. Uzoefu unaonyesha kwamba, katika kipindi kama hiki cha sikukuu kuna baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na endapo vitajitokeza viweze kudhibitiwa kwa haraka.Aidha, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Vilevile, Jeshi la Polisi linawataka madereva na watu wote watakaokuwa wakitumia barabara, kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka kwenda mwendo kasi, kujaza abiria kupita kiasi na kutumia vilevi wawapo kazini. Wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.

Aidha, wazazi wawe makini na watoto wao, kutokuwaacha watembee peke yao ama kwenda disko toto bila kuwa chini ya uangalizi wa watu wazima ili kuepusha ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.

Wananchi wakumbuke kutokuacha makazi yao bila uangalizi na endapo italazimu kufanya hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya, watoe taarifa haraka kwenye vituo vya polisi vilivyo karibu yao, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

Mwisho, Jeshi la Polisi linapenda kuwashukuru wale wote ambao tayari wamefunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya biashara hususani yale yanayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu, yakiwemo maduka, mahoteli na maeneo ya benki. Jeshi la Polisi linaendelea kuwasisitiza ambao bado hawajaweka kamera hizo, kuweka ili ziweze kusaidia kubaini wahalifu na hata kurahisisha ukamataji wa wahalifu hao endapo uhalifu unatokea.

Tunawatakia Watanzania wote Pasaka njema.

Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi
HABARI KAMILI..>>>

Taarifa ya mabadiliko ya uelekeo wa barabara jijini Dar.....

MABADILIKO YA UELEKEO WA BARABARA KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM KUANZIA SIKU YA TAREHE 28/04/2014. (TRAFFIC CIRCULATION AT CBD)

Ufunguo wa ramani iliyopachikwa hapo juu:-
  1. RANGI YA NJANO - Njia ya uelekeo mmoja (One Way)
  2. RANGI YA BLUE MPAUKO - Njia ya mielekeo miwili (Two Way)
  3. RANGI YA KIJANI - Mitaa ya kutembea kwa miguu, magari marufuku (Walking streets)
  4. RANGI NYEKUNDU - Barabara za kupita daladala
  5. RANGI YA BLUU ILIYOIVA - Barabara za DART
  6. DUARA ZA NJANO - Mzunguuko (Round-about)
  7. MSALABA WA KIJANI - Makutano yenye taa za kuongozea Magari (Signalized intersection)
1. Kipande cha Mtaa wa Samora kuanzia Mnara wa Askari (Askari Monument) hadi Clock Tower. Magari kutakuwa na mabadiliko ambayo magari yatakuwa yanaelekea Clock Tower badala ya Askari Monument.
 
2. Barabara ya Sokoine kuanzia Station hadi makutano ya Mtaa wa Maktaba, Posta ya Zamani, magari  yatakuwa yanaelekea Uelekeo mmoja wa Station, Posta ya Zamani tofauti na ilivyo sasa Posta ya Zamani kwenda Station. 

3. Barabara ya Kivukoni kuanzia Posta ya Zamani hadi ferry itakuwa barabara ya mielekeo miwili (Two Ways).

4. Barabara ya Samora kuanzia mnara wa Askari hadi Ocean Road Hospital itakuwa ni barabara ya mielekeo miwili.
 
5. Daladala zote zitakazotokea barabara za Makataba zitakunja kulia pembeni ya jengo la NBC na hadi makutano ya Mkwepu na kukunja kushito kuingia Sokoine pale Posta ya Zamani na baadaye kukunja kushoto kuingia Makataba na kurudi Posta Mpya.
 
Kwa Maelezo zaidi Wasiliana na Ofisi za DART zilizopo UBUNGO PLAZA GHOROFA YA KWANZA au kwenye OFISI YA MHANDISI WA MANISPAA YA ILALA, mkabala na SHOPRITE SUPERMARKET, jirani na KAMATA.

Mtaarifu mwingine juu ya mabadiliko haya kuondoa usumbufu ifikapo siku ya Jumatatu 28/04/2014.
 
HABARI KAMILI..>>>

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 kuahirishwa....“Nikiri nafasi ni finyu sana ila tutalizungumza serikalini,” asema Rais Kikwete


UCHAGUZI wa serikali za mitaa, ambao hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, huenda usifanyike mwaka huu, imeelezwa.

Hatua hiyo inatokana na uchaguzi huo kuingiliana na masuala ya kupata Katiba mpya, ambayo mchakato wake bado unaendelea.
 
“Nikiri nafasi ni finyu sana ila tutalizungumza serikalini,” alisema Rais Jakaya Kikwete, alipozungumza na baadhi ya wahariri Ikulu mjini Dar es Salaam juzi.

Rais Kikwete alisema atakutana na viongozi wengine wa serikali ili kuamua kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa kama ufanyike mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyo kawaida au la.
 
Alisema ni kweli nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi huo ni finyu sana kwa kuwa suala la Katiba mpya litaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu kipindi ambacho uchaguzi huo huwa ukifanyika.
 
Iwapo uchaguzi huo utaahirishwa, huenda ukafanyika mwakani na uchaguzi mkuu, lakini tofauti na ilivyozoeleka, upigaji kura utakuwa nne kwa Tanzania Bara.
 
Kwa kawaida upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu unahusisha kura ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kura kwa ajili ya mbunge na kura ya diwani.
 
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza wasiwasi wake kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
 
Pinda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni kuwa, muda uliopangwa kwa ajili ya Bunge Maalum ni siku 70, lakini kazi ilikuwa ikienda kwa kusuasua.
 
“Hatari ya kusogeza mbele uchaguzi wa serikali za mitaa ninaiona dhahiri, nadhani itabidi tu tumuombe Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, tusogeze mbele uchaguzi huu, ili kutoa nafasi kwa kazi zingine kuendelea hususan ya kutengeneza katiba,” alisema Pinda.
 
Pinda alisema pia kuwa iwapo kazi ya bunge hilo itakuwa haijamalizika ifikapo mwishoni mwa Aprili mwaka huu, watamuomba Rais Kikwete aliahirishe ili lipishe Bunge la Bajeti liendelee na kazi zake.
 
“Hatuwezi kuacha kazi zingine za serikali zikasimama, lazima ziendelee, na zitaendelea kama bajeti za wizara zitapitishwa, nadhani kama hatutakwenda sawa, tutamuomba tu Rais aahirishe bunge hili la Katiba, tufanye kazi hii nyingine iliyo mbele yetu,” alisema Pinda. 


Credit: Gazeti  la  Uhuru 
HABARI KAMILI..>>>

Stephen Wasira afunguka....Asema hashangazwi na kitendo cha kutoka nje ya bunge wajumbe wa UKAWA kwani, ni matukio yaliyopangwa muda.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, amesema hakushangazwa na kitendo cha kutoka nje ya bunge wajumbe wa UKAWA kwani, ni matukio yaliyopangwa muda.

Wasira alisema UKAWA walikuwa na mpango huo muda mrefu baada ya kuona hoja yao kuhusu kutokuwepo kwa hati ya muungano kukosa ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wasira alisema sababu wanayosema kuwa wametukanwa ndipo wakaamua kutoka nje ya bunge, haina mashiko kwani UKAWA walitoa maneno ya kashfa dhidi ya waasisi wa Muungano.
 
“Hoja iliyotolewa na Kiongozi wa UKAWA kuwa wanatukanwa bungeni ni ya ajabu kwa kuwa UKAWA wamekuwa wakiwatolea maneno yasiyofaa waasisi wa muungano, kitendo ambacho hakikubaliki na Wananchi” alisema 
 
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wajumbe wa bunge hilo kushindana kwa hoja na sio kutoka nje ya bunge na kutafuta sababu zisizokuwa na msingi. 
HABARI KAMILI..>>>

Mwigulu Mchemba asimamisha malipo ya posho ya wabunge wote waliosusia vikao vya bunge juzi


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Mchemba amesema serikali imesimamisha malipo ya posho ya wabunge wote waliosusia vikao vya bunge juzi.

Pia, amesema wajumbe ambao ni watumishi wa umma, wataripotiwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
 
Alisema licha ya kuwa wajumbe hao wameshalipwa posho hizo hadi Aprili 26, mwaka huu, tayari amesitisha malipo hayo ambayo yalikuwa yapitie benki.

“Huku kwa upande wa bunge taratibu za kuwalipa zilishakamilika, lakini kwa kuwa malipo hayo yanapitia benki, nimeagiza wasitishe,’’ alisema.
 
Alisema malipo kwa wajumbe hao yatafanyika pale tu watakaporejea ndani ya bunge kuendelea na mchakato huo wa Bunge.
 
“Watakaolipwa posho kwa sasa ni wale wanaohudhuria vikao, hatuko pikiniki hapa, tunawalipa watu halafu hawataki kufanya kazi,” alisema.

Juzi, Livingstone Lusinde alisema kilichokosewa ni uamuzi wa bunge kulipwa kwa fedha za sikukuu, jambo ambalo limewafanya kususa na kuondoka.
 
Naye Said Mkumba alielezea kushangazwa na wajumbe hao walioamua kutoka nje, akihoji kwamba kwa nini hawakutoka siku mbili zilizopita, mpaka wamesubiri walipwe posho hadi ya Aprili 26, ndio waondoke. 
HABARI KAMILI..>>>

Martin Kadinda amwita Lulu Michael Nyau


Mwanamitindo maarufu Bongo, Martin Kadinda amempongeza Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwa kumuita nyau.
 
Martin alifanya ishu hiyo wakati akimtakia Lulu Happy Birthday Aprili 16 ambapo mwanadada huyo alikuwa akitimiza umri wa miaka 19. Mwandishi wetu alipomhoji kuhusiana na kumuita nyau, Martin alifunguka:
 
“Yule kwangu ni mdogo, nimemlea tangu akiwa anasoma sekondari pale Perfect Vision Ubungo, nimetumia neno nyau kama utani lakini nikimaanisha mdogo kwangu.”
HABARI KAMILI..>>>

Magazeti ya leo Ijumaa ya tarehe 18 April 2014

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Magazeti  ya  leo  Ijumaa  ya  tarehe  18  April  2014
HABARI KAMILI..>>>

Rais Kikwete akerwa na kitendo cha wanasiasa kumtukana Mwalimu Nyerere....Asema ni utovu wa nidhamu kuwatukana waasisi wa Tanzania

Rais Jakaya Kikwete amesema ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu unaoonyeshwa na baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waanzilishi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. 
 
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa kwenye mahojiano maalumu na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari (wa Mwananchi hawakuwapo) ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.
 
Kauli hiyo ilikuwa ni jibu la moja ya maswali alilokuwa ameulizwa na wahariri hao kuhusu matusi, kejeli na dhihaka ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na wabunifu wakuu wa Muungano wa Tanzania.
 
“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki au kuwakejeli waasisi wa Taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo makubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
 
“Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale Tanzania Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi, bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
 
Rais alisisitiza kuwa ni ukosefu wa adabu kwa yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.
 
“Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii,” alisema.
 
Wakati huo huo, Rais Kikwete alipokea rasmi tuzo ya Kiongozi Bora wa Maendeleo Afrika –kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyeipokea kwa niaba yake huko Marekani, Aprili 9, mwaka huu.
 
Rais Kikwete alisema amepokea tuzo hiyo na amewazawadia Watanzania wote, kwa sababu wao ndiyo waliochangia maendeleo yaliyomwezesha kupata heshima hiyo.
 
“Napokea Tuzo hii kwa niaba ya Watanzania wote. Aidha, naitoa kwa Watanzania kwa sababu, hata kama nimekuwa kiongozi, ukweli ni kwamba mafanikio na maendeleo yote yaliyopatikana hadi kutunukiwa tuzo hii, yametokana na juhudi zetu za pamoja,” alisema.
HABARI KAMILI..>>>

Thursday, April 17, 2014

UKAWA wamegoma kabisa kuhudhuria mkutano wa bunge maalum la katiba


Umoja wa katiba ya wananchi bungeni -UKAWA- umegoma kabisa kuhudhuria mkutano wa bunge maalum baada ya kutoka katika mkutano uliofanyika Aprili 16 kwa madai ya mkutano huo kugubikwa na matusi, kashfa na vitisho vinavyofanywa na baadhi ya viongozi kwa wananchi. 
 
Akizungumzia masikitiko yake mwenyekiti wa kamati ya bunge maalum, Mhe. Samweli Sita amesema licha ya bunge hilo kumwita bungeni Mhe. William Lukuvi kutoa ufafanuzi wa tuhuma  zinazomkabili  ameutaka UKAWA  kuja katika kamati ya uongozi kueleza kwa undani nini hatma ya maamuzi yao.
 
Akiitikia wito wa kuitwa bunge hilo,waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera uratibu na bunge, Mhe. William Lukuvi ameeleza hofu yake kuhusu muundo wa serikali tatu  na kulieleza bunge dhamira ya vyama vikuu vya upinzani vya kugawana Tanganyika na Zanzibar.
 
Wakitoa maoni yao nje ya bunge, baadhi ya wabunge wameutaka umoja huo kuitikia wito wa wenyekiti wa bunge hilo wa kuhudhuria mikutano kama kawaida na kupeleka malalamiko yao kwa kamati ya uongozi ili kutafuta njia bora ya kufikia mwafaka na kuwapatika wananchi katiba mpya. 
 
ITV imeutafuta uongozi umoja wa katiba ya wananchi-UKAWA uliokuwa ukifanya mkutano wake wa ndani na kuzungumza na mwenyekiti wa umoja huo Mhe Freeman Mbowe ambae amepinga kauli ya kiongozi huyo wa serikali kudai kuwa ni hofu yake binafsi na kusisitiza baadhi ya vinongozi wengine wameshawahi kutoa kauli kama hiyo ambapo ametoa msimamo wa umoja huo.

Credit: ITV
HABARI KAMILI..>>>

Mwanafunzi wa chuo cha IFM akamatwa na Bangi kilo 50


Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia abiria wa tatu waliokuwa wakisafiri na Basi la New Force kutoka Kahama kuelekea Jijini Dar es Salaam.Wanaoshikiliwa ni Kevin Prospar(aliyekaa pichani kulia),Joseph Charles (aliyekaa kulia) na John Joseph(aliye kaa katikati)
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime kushoto akikagua bangi iliyo kamatwa.
Basi la New Force lililokamatwa likiwa limebeba abiria waliokuwa na bangi likiwalimeshililiwa kwa muda Makao ya Polisi Mkoa wa Dodoma.
 *********
By Geofrey Adroph via Pamoja Pure blog -- Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linawashikilia watu watatu kwa kosa la Kupatikana na bhangi kiasi cha Kilogramu 133.5 yenye thamani ya Ths. 20,025,000/= bei ya mitaani (street value).
 
Watuhumiwa hao wamekamatwa mnamo tarehe 16/04/2014 majira ya 7:30 mchana eneo la Stendi Kuu ya mabasi katika Manispaa na Mkoa wa Dodoma. 

Watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha bhangi katika mabegi baada ya kupanda basi kutokea Kijiji cha MANONGA – TINDE Mkoani SHINYANGA kwenda jijini Dar es Salaam katika basi namba No. T.931 CGU mali ya kampuni ya NEW FORCE linalofanya safari zake kutokea Kahama kwenda jijini Dar es Salaam. 
 
Watu hao walifahamika kwa majina ya:-
  1. CALVIN S/O PROSPER SALEKA, miaka 23, kabila Mchaga, Mwanafunzi wa chuo cha Institute of Finance Management (IFM) cha Dar es Salaam, mwaka wa pili, alikamatwa akiwa na mabegi mawili ya bhangi yenye uzito 51kgs.
  2. JOHN S/O JOSEPH, Miaka 31, kabila Msukuma, mkulima na mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, alikamatwa akiwa na mabegi mawili ya bhangi yenye uzito wa 42.5kgs.
  3. JOSEPH S/O CHARLES BATONI, Miaka 22, kabila Msukuma, mkulima na mkazi wa Shinyanga. alikamatwa akiwa na mabegi mawili ya bhangi yenye uzito 36.5kgs
Watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia taarifa za raia mwema aliyewatilia mashaka na kutoa taarifa Polisi. Mbinu waliyotumia kusafirisha ni kuhifadhi katika mabegi makubwa ya nguo na kufunga kwa mifuko ya nailoni kisha kusaga vitunguu na kuweka katika mabegi hayo pamoja na kupulizia manukato (perfume) ili kuondoa harufu wasiweze kugundulika kirahisi.

Tukio lingine katika kijiji cha Central Kiteto Tarafa ya Mlali Wilaya ya Kongwa zilikamatwa lita 300 za Pombe haramu ya Gongo nyumani kwa Salumu s/o Chamagulu ambaye alikimbia baada ya kuona Polisi na tunaendelea kumtafuta.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi David A. Misime – SACP, anawapongeza kwa dhati raia wema wanaoshirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuendelea kudhibiti madawa ya kulevya na Pombe ya Moshi inayoharibu vijana wengi.
HABARI KAMILI..>>>

Magazeti ya leo Alhamisi ya tarehe 17 April 2014

 
 
 
 
 


 

 

 

 

 

 

 

 

 


 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 

Magazeti  ya  leo  Alhamisi  ya  tarehe  17  April  2014

HABARI KAMILI..>>>