Friday, March 25, 2016

Mwanafunzi Afa kwa Kupigwa na radi Porini Alikokuwa Amejificha


Mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Swaila, kata ya Mkwamba wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Maria Pangani (14) amekufa papo hapo baada ya kupigwa radi.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma kupitia Mpango wa Memkwa, alipigwa na radi akiwa amejificha porini baada ya mama yake kumtishia kuwa atafikishwa katika Serikali ya kijiji hicho baada kugundua kuwa alikuwa akiimiliki kwa siri simu ya kiganjani bila kufahamika aliyemnunulia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarunda alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Machi 22 , saa 11:00 jioni katika kijiji cha Swaila wilayani Nkasi.

Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Swaila, Juvenary Mmanzi alisema, mama mzazi wa mtoto huyo alishangaa kuona binti yake akiwa na simu.

“ Ndipo mama yake alipomhoji alikoipata simu hiyo, binti alikataa kumtaja mtu aliyemnunulia ndipo mama yake alipohamaki na kumtishia kuwa atampeleka katika Serikali ya Kijiji afungwe asipomtaja mtu aliyemnunulia simu hiyo “ alieleza Mmanzi.

Kwa mujibu wa Mmanzi, mtoto huyo alijawa na hofu kubwa ya kufungwa jela akakimbilia porini kujificha na ghafla mvua ilianza kunyesha na ndipo alipigwa na radi.

Inadaiwa kuwa, wakazi wa kijiji hicho walifika kwenye pori hilo na kukuta mwili wa marehemu ukiwa umeunguzwa.

Simu na matunda aina ya mapera vilikutwa kwenye mfuko wa sketi aliyokuwa ameivaa.

Kwa mujibu wa Mwaruanda, uchunguzi wa kitabibu umeonesha kuwa kifo cha mtoto huyo kimesababishwa na radi iliyompiga, mwili wake ulikabidhiwa kwa wazazi wake kwa maandalizi ya maziko.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )