Tuesday, March 22, 2016

Rais Magufuli Atuma Salamu Za Rambirambi Kufuatia Vifo Vya Wafanyakazi Sita Wa Bagamoyo Waliofariki Ajalini


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, kufuatia vifo vya wafanyakazi sita wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, vilivyosababishwa na ajali ya barabarani, iliyotokea leo tarehe 21 Machi, 2016 katika eneo la Kerege Wilayani humo.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa tano za asubuhi, baada ya Lori la kubebea mchanga kuyagonga magari mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambayo yalikuwa katika Msafara wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na serikali za mitaa, iliyokuwa akitoka kukagua mradi wa Maji wa Mapinga.

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za vifo vya wafanyakazi hao wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ambao wamepoteza maisha wakiwa wanatekeleza majukumu ya kikazi.

“Kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Pwani naomba kutoa pole nyingi kwa familia za marehemu wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo, naomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu kutokana na kuondokewa na wapendwa wao” Amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi. Amina

Aidha, Rais Magufuli amewapa pole wafanyakazi wengine wanane ambao wameumia katika ajali hiyo, na amewaombea wapone haraka.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
21 Machi, 2016

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )