Thursday, March 24, 2016

Waziri Nape Atuma Salam Za Rambirambi Kufuatia Kifo Cha Aliekuwa Mkuu Wa Wilaya Ya Njombe, Marehemu Sara Dumba


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ametuma salamu za rambirambi kwa  wanahabari wote kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe na  Mtangazaji Mwandamizi wa zamani wa Redio Tanzania (RTD), Dar es salaam  Marehemu Sara Dumba.

“Pokeeni salamu za rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na  Mwanahabari  mahiri Bi. Sara Dumba aliyekuwa mfano wa kuigwa” amesema Mhe. Nape.

“Mbali na utangazaji wake mahiri, Bi. Sara Dumba alikuwa mzalendo wa kweli aliyetumikia tasnia hii ya Habari na Serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake. Ni wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”.

“Hakika Sara tutamkumbuka, nawapa pole wananchi wote wa wilaya ya Njombe kwa kuondokewa na kiongozi wao mpendwa  mwenzao”,ameongeza Waziri Nape.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante  Ole Gabriel  naye ametuma salamu hizo “Salaam ziwafikie familia, ndugu jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu ambao unawagusa sana, naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa pamoja ni wakati wa kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”,amesema Profesa Elisante na kuwatakia moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Baadhi ya wafanyakazi wenzake waliowahi kufanya kazi  pamoja naye ambao ni Aloisia Maneno amesema Bi. Sara alikuwa mwalimu wake katika masuala ya utangazaji kwa kuwa ndiye aliyemfundisha jinsi ya kuandaa kipindi cha watoto  cha Cheichei  Shangazi.

Abdul Ngarawa  amesema kuwa Bi. Sara alikuwa mchapakazi hodari, mtu mwenye kipaji cha utangazaji, mcheshi, mtu mwenye ushirikiano na wafanyakazi wenzake na jasiri asiyeogopa kusema ukweli hata kwa wakuu wake wa kazi pale ambapo kazi hazikufanyika vizuri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Hajjat Halima Kihemba akizungumzia uhusiano wake na marehemu amesema kwamba yeye alianza kazi RTD  mwaka  1971 ambapo Bi. Sara alimkuta tayari akiwa kazini kati ya mwaka 1974, hivyo walifanya naye kazi pamoja kwenye Idhaa ya Kiingereza ya (External Services) marehemu akiwa  msaidizi wake.

   “Alikuwa ni mtu  mwenye mchango mkubwa na yuko tayari kufanya kazi wakati wote  unapomwihitaji usiku na mchana, mshauri hususan kwa watoto wa kike kuacha kujidharau na kuona kwamba hawezi kufanya kazi ya taaluma ya habari na mtu aliyependa maendeleo.

Kwa  upande wake, Bakari Msulwa ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma - TBC akimzungumzia  Bi.Sara Dumba amesema kuwa alihamishiwa mkoani Morogoro  mwaka 1990 akiwa mwakilishi wa RTD  na baade Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma  hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mwaka 2006 .Ameongeza kwamba ni mama aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake, aliandaa vipindi mbalimbali vya biashara na alikuwa yuko tayari kuambiwa ukweli.

“ Kwa kweli Bi. Sara alijenga historia nzuri katika tasnia  ya masuala ya habari na utumishi wa umma akiwa katika ngazi ya ukuu wa wilaya, hivi karibuni nilionana naye mkoani Tabora miezi miwili iliyopita alikuwa na mtazamo wa kuwaunganisha  wafanyakazi wa RTD  ili waweze kuwa na umoja utakaoweza kutupatia nafasi ya kusaidiana kwenye masuala mbalimbali,” Amesema  Msulwa.

 Msulwa amebainisha kuwa Bi. Sara alisema hayo baada ya  kubaini kwamba  hakuna historia ya wafanyakzi wa RTD. Hivyo ameacha changamoto  kwa hao  kuacha historia zao  ili  ziweze kuwa na manufaa kwa watu wengine.

Bi. Sara amefariki   dunia tarehe 21 Machi,  mwaka 2016 Wilayani Njombe,  baada  kuugua ghafla.  Alizaliwa Oktoba 19, 1956. Bi. Sara alianza kazi katika Radio ya Taifa, Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD) na baadaye Shirika la Utangazaji Taifa (TUT) sasa TBC.

Marehemu  Sara Dumba kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya mwaka 2006 alivuma katika kipindi cha Majira(yaani habari za hapo kwa hapo) na vipindi vingine vingi.

 Kwa mujibu wa taarifa za Katibu Tawala wa  Mkoa wa Njombe Jackson  Saikadau  amesema mwili wa marehemu  unatarajiwa kuagwa kesho Machi 24, mwaka huu  jijini Dares Salaam na kuzikwa nyumbani kwake eneo la  Mbutu  Mwembe Mdogo, Kigamboni.

Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.

IMETOLEWA NA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
23, MACHI, 2016.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )