Thursday, April 14, 2016

Watumishi HEWA Wakopa Mamilioni ya Pesa Benki......TAMISEMI Mwanza Yaongoza kwa Rushwa

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha Mkoani Mwanza  Mhandisi Ernest Makale
*******

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, imebaini kuwepo kwa watumishi hewa zaidi ya watano ambao uongozi wa mkoa huo haukuyawasilisha majina yao kwa Rais Dk. John Magufuli huku yakionekana kukopa fedha benki.

Pia Takukuru imesema kuwa majina ya watumishi hewa hao baada ya kufanya uchunguzi wamebaini hukopeshwa fedha kwa kisingizio kwamba wao ni watumishi wa Serikali kitendo ambacho ni cha uongo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale wakati akitoa taarifa ya robo mwaka kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ambako alisema  majina yaliowasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella sio kamilifu.

Amesema watumishi hao hewa wamekuwa wakikopa fedha kutoka benki mbalimbali kwa kutumia nyaraka za kughushi jambo ambalo alidai kwamba kuna baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanaohusika kufanya udanganyifu huo.

Amesema pia katika uchunguzi wao unaonesha kuwa majina ya watumishi yaliowasilishwa na baadhi ya halmashauri za mkoa huo sio kamilifu kwani kuna watumishi wengine ambao hawajaorodheshwa.

Makale amesema kuwa kutokana na kuonekana kwa hali hiyo Takukuru inaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watumishi hewa wengine na watumishi wengine wanaoshirikiana nao.

“Kuna dalili za wazi ambazo zinaonesha kuna watumishi wasiokuwa waaminifu wa halmashauli ambao wanahusika kufanya vitendo hivi vya udanganyifu, atakaebainika atafikishwa mahakamani,” amesema Makale.

Watumishi wadakwa kwa utapeli
Makale pia amesema kuwa Takukuru Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha miezi hiyo tayari imewakamata aliyekuwa Meya wa Ilemela, Henry Matata, Justine Lukaza (Mhandisi wa Manispaa ya Ilemela) na Mfanyabiashara, Hemed Hamad kwa kosa la kutoa zabuni feki ya kutoza ushuru kwenye stendi ya mabasi ya Buzuruga jijini hapa.

Watumishi wengine waliokamatwa kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao ni pamoja na aliyekuwa Mganga wa Wilaya ya Magu, Patrick Mwindunga, Afisa Ugavi wa Wilaya ya Misungwi, Zabron Marwa, anaetuhumiwa kuingia manunuzi feki.

Wengine ni wauguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Masalu Kangalukwi na Amon Shija wanaotuhumiwa kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagonjwa.

TAMISEMI yaongoza kwa Rushwa
Katika taarifa hiyo, Mhandisi Makale amebainisha kuwa Takukuru imepokea jumla ya malalamiko 45 yanayohusiana na vitendo vya rushwa kutoka kwa wananchi ambapo katika malalamiko hayo, 27 yameelekezwa kwa watumishi wa idara za Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 60. Kati ya malalamiko hayo 27, malalamiko 13 yameelekezwa katika idara ya ardhi.

Amesema idara zinazofuata kwa kulalamikiwa ni Mahakama yenye malalamiko tisa, polisi malalamiko sita na idara ya afya malalamiko matatu.

Mhandisi Makale amesema kesi 33 zinaendelea Mahakamani kutokana na vitendo vya rushwa Mkoani Mwanza huku kesi sita zikiwa ni mpya katika kipindi cha miezi mitatu na nyingine zikiwa katika upelelezi. 

==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )