Monday, May 23, 2016

CCM: Hatutamuadhibu Kitwanga Mara Mbili

CCM imesema kitendo cha Rais John Magufuli kumvua uwaziri Charles Kitwanga kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa, kimedhihirisha kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, lakini hakitachukua hatua kwa kuwa ameshaadhibiwa.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka jana  alisema kitendo cha Kitwanga kuingia bungeni akiwa amelewa kimewapa fundisho na sasa wanajua kuwa kuna baadhi ya watumishi waliopewa dhamana na chama hicho, lakini wanakiuka miiko ya maadili ya utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume na taratibu zao.

Sendeka alisema licha ya kwamba Rais Magufuli amechukua hatua juu ya hilo na kutoa adhabu, CCM itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wanasiasa waliopewa dhamana na chama hicho.

“Hatutasita kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kada anayekiuka maadili ya viongozi wa umma,” alisema Sendeka.

Alisema CCM inampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi aliochukua dhidi ya Kitwanga kwa kuwa hatua hiyo imedhihirisha kauli aliyowahi kusema kwamba hataangalia mtu usoni wala kujali kabila au dini, ikiwa mtu huyo atakiuka miiko ya uongozi.

Kuhusu CCM kumuadhibu Kitwanga, Sendeka alisema adhabu aliyopewa na Rais inatosha. “Hukumu haitolewi mara mbili,” alisema Sendeka.

Kitwanga ambaye anatajwa kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, alivuliwa ukuu wa wizara hiyo nyeti baada ya kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge Ijumaa asubuhi na kujibu maswali akiwa amelewa.

Hadi jana jioni, Rais Magufuli alikuwa bado hajajaza nafasi hiyo nyeti huku wananchi wakibashiri jina la mrithi wa Kitwanga kwa kuangalia jinsi marais waliopita walivyokuwa wakijaza nafasi kama wa kumpandisha naibu waziri wa wizara hiyo au nyingine, kumteua mtu anayemfahamu, kubadilisha mawaziri na kumrejesha aliyewahi kuwa waziri ama kuteua kutoka kwenye kanda anayotoka aliyetimuliwa.

Mara nyingi katika uteuzi wa mawaziri, viongozi wakuu wa nchi wamekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.

Mara zote saba ambazo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri alifuata utaratibu huo.

Alipomuondoa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mbunge kutoka mkoa Kagera alimteua mbunge mwingine kutoka mkoa huo, Charles Mwijage kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.Kwa sasa Mwijage ni Waziri wa Viwanda na Biashara. 

Utaratibu huo unaweza kunufaisha wabunge sita wa majimbo yaliyopo mkoa wa Mwanza ambao ni Chalres Tizeba (Buchosa), Mansoor Hirani (Kwimba), Kiswaga Boniventura (Magu), Stanslaus Mabula (Nyamagana), William Ngeleja (Sengerema) na Richard Ndassa (Sumve).

Mbali na Kitwanga ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka mkoa huo, Rais pia alimteua mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Iwapo Rais atatumia utaratibu wa kupandisha naibu waziri kuwa waziri, neema huenda ikamuangukia mbunge wa Kikwajuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandishi Hamad Masauni au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine. Katiba pia inampa Rais fursa ya kuteua wabunge 10 na tayari ameshatumia nafasi sita.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )