Saturday, June 4, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Ya Nchi , Hamad Yussuf Masauni Alalamikiwa na Wabunge Kwa Kutoa Majibu ya Dharau na Kiburi Kwa Wabunge

SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kutokana na ulevi, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Yussuf Masauni, ameshtakiwa kwa uongozi wa Bunge akidaiwa kutoa majibu ya dharau bungeni.

Wakati wizara hiyo bado haijapata Waziri tangu 'kutumbuliwa' kwa Kitwanga Mei 20, mwaka huu, katika Kikao cha 36 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 mjini hapa, jana Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Keissy alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akidai Mhandisi Masauni amekuwa akitoa majibu ya dharau kwa wabunge.
 
Keissy alidai Naibu Waziri huyo amekuwa akitoa majibu ya kejeli na kiburi na kwamba wabunge wengi hawaridhishwi na majibu yake.
 
"Nasimama kwa Kanuni ya 68(7), naomba mwongozo wako kuhusu majibu ya nyongeza aliyojibu Naibu Waziri, na tangu jana (juzi), amezoea kujibu kwamba wabunge watumie fedha za mfuko wa Jimbo kukarabati majengo ya polisi," Keissy alisema.
 
"Ndugu Mheshimiwa Naibu Spika, majengo ya Karando na Kabwe (jimbo la Nkasi) yamechakaa hata mfuko wa jimbo... nadhani Mheshimiwa Waziri hajui tunapata shilingi ngapi za mfuko wa jimbo kutosha kukarabati hayo majengo.
 
"Hayo majibu yanaridhisha? Anajibu kwa jeuri na kiburi. Kusema kweli wabunge haturidhishwi na majibu ya Naibu Waziri. Sikubalini na majibu ya aina hii. 
 
"Katika majibu ya msingi ya swali langu, wamesema serikali itakarabati majengo ya Kabwe, lakini anasema baadaye (kwenye swali la nyongeza) Mbunge akarabati majengo ya Kabwe, si dharau hii? Anataka kunichionganisha mimi na wananchi. Hili jibu sijaridhika nalo. Mnanijibu nikakarabati mimi. Sina uwezo."
 
Baada ya maelezo hayo ya Keissy, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alisema atatoa mwongozo wake baada ya kupitia taarifa za Bunge (Hansard) kuhusu suala hilo.
 
"Waheshimiwa wabunge, ili nijue swali liliulizwa kwa namna gani na Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibu kwa namna gani, mpaka nipitie taarifa za Bunge, yaani Hansard," alisema Naibu Spika. 
 
"Kwa hiyo, mwongozo huo nitautoa baada ya kupitia taarifa rasmi za Bunge kwamba swali liliulizwa vipi na majibu yametoka namna gani."
 
Ikiwa Kiti cha Spika kitabaini majibu ya Naibu Waziri hayakusadifu swali la Keissy, kitaagiza swali hilo lirudiwe kujibiwa kwenye kipindi cha maswali na majibu bungeni.
 
Uteuzi wa Kitwanga ulitenguliwa na Rais Magufuli ikiwa ni muda mfupi baada ya Mbunge huyo wa Misungwi (CCM) kuingia bungeni akiwa amelewa na kijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja lililoelekezwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Kiti cha Spika kiliagiza swali hilo lirudiwe kujibiwa katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Mei 23, baada ya Kitwanga kutoa majibu ambayo hayakuridhisha.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )