Wednesday, June 1, 2016

Serikali Yatoa Ufafanuzi Uboreshaji wa Maslahi ya Polisi na Nafasi za JKT

Serikali imesema kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi na kuwajengea nyumba za kisasa za kuishi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina wakati akijibu maswali ya wabunge kuhusu mkakati wa Serikali wa kuboresha maslahi ya Askari wa Jeshi hilo kwa niaba ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Bungeni mjini Dodoma leo
 
Amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 itatekeleza Mpango kabambe wa ujenzi wa nyumba za Polisi 4136 ambao utakwenda sambamba na ujenzi wa vituo vya Polisi.

Amesema Serikali imechukua hatua za haraka kulishughulikia suala la ukosefu wa nyumba za askari hao katika maeneo mbalimbali nchini ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yenye ukosefu wa nyumba hizo.

Amelieleza Bunge kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa maslahi ya Askari Polisi yanaimarishwa ikiwemo malipo ya Posho ya pango kwa askari wasio na nyumba ambayo ni asilimia 15 ya mishahara yao ili waweze kulipia gharama hizo.

Ameongeza kuwa  askari wenye utalaam maalum wakiwemo madereva na madaktari wamekuwa wakilipwa posho ya asilimia 15 ya mishahara yao na kuongeza kuwa askari wanaoajiriwa katika ajira mpya kama madaktari wamekuwa wakilipwa mishahara sawa na madaktari wengine bila kujali vyeo vyao.

“Serikali tumefanya jitihada kubwa sana kuboresha maslahi ya askari wetu, kama Serikali tumetoa posho za nyumba, posho za utalaam maalum kwa askari wote ambayo ni asilimia 15 ya mshahara wa kila Polisi hii yote ni kuwafanya askari wetu waweze kumudu gharama za maisha” Amesisitiza Mhe. Mpina.
 
Ameeleza kuwa kwa askari wanaofanya kazi katika mazingira magumu wakiwemo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamekuwa wakipewa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu (Hardship allowance) kiasi cha shilingi laki moja (100,000) kila mwezi.
 
Mhe. Mpina amebainisha kuwa askari wote wanaohitimu mafunzo yao wamekuwa wakikatiwa Bima ya Afya kwa asilimia 100 na Serikali pamoja na udhamini wa mikopo mbalimbali katika taasisi za kifedha ili waweze kupewa mikopo na taasisi hizo.
 
Aidha, amesisitiza kuwa serikali imewapandishia kiwango cha Posho ya katikati ya mwezi (Ration Allowance) kutoka shilingi 180,000 za awali hadi 300,000 ambazo wanalipwa kwa sasa nchi nzima.
 
Katika hatua nyingine Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imetoa ufafanuzi kuhusu vijana wa kidato cha nne kutochukuliwa kujiunga na  Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
 
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi  amesema kuwa hatua ya kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa haiwezekani kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa Serikali.
 
Amesema kuwa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea kwa sasa ni 5000 hadi 7000 kwa mwaka kulingana na bajeti inayotolewa na kuongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha na kujenga kambi zaidi za mafunzo ili kuwawezesha vijana wengi kujiunga  na mafunzo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha.
 
Kwa upande wa wahitimu wa kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na JKT kwa mujibu wa Sheria Mhe. Mwinyi amesema Serikali imewachukua vijana 14,000 na inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kuchukua vijana wengi zaidi.
 
Amesema Serikali inakusudia kujenga majengo ndani ya makambi ili kuwezesha vijana wote wanaohitimu kidato cha sita kupitia JKT kabla ya kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.
 
Aidha, Amefafanua kuwa kwa wale wanaojiunga na JKT kwa kujitolea ambao idadi yao inafikia 5000 sio wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa katika vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuongeza kuwa ni asilimia 71 ndio hupata ajira kwenye vyombo hivyo huku waliobaki wakilazimika kurudi nyumbani.
 
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia utaratibu wa kuwawezesha vijana hao ili wanaporudi uraiani waweze kupatiwa mitaji ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )