Saturday, June 4, 2016

Waziri Mpango: Tutaendelea Kukopa ili Tuendelee

WAKATI deni la Taifa likifikia zaidi ya Sh trilioni 35, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango amesema Tanzania ina mahitaji makubwa ya maendeleo yanayoilazimu kuendelea kukopa, kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa vya uhimilivu wa deni.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo ya Sh trilioni 9.5, Dk Mpango alisema kwa kuwa lazima taifa likope ili kuleta maendeleo, ni lazima taifa liwe na madeni.

“Nchi yetu ina mahitaji makubwa ya maendeleo hivyo lazima tukope na ukikopa, unaingia katika madeni,” alisema na kufafanua mambo ya msingi yanayozingatiwa na Serikali wakati wa kukopa.

Jambo la kwanza wanalozingatia kwa mujibu wa Dk Mpango ni masharti ya mkopo, yanayojumuisha riba ambapo wanaangalia riba hiyo ni kiasi gani; muda wa kuanza kulipa baada ya kuchukua mkopo (grace period) na utaratibu wa malipo.

Suala la pili la msingi kwa mujibu wa Dk Mpango, ni mahali fedha hizo za mkopo zinakopelekwa ambapo alifafanua kuwa ukopaji wa Serikali hauna tofauti na ukopaji wa mtu binafsi, ambaye akielemewa anakaribisha matatizo.

Dk Mpango alisema Tanzania inakopa kwa ajili ya kutengeneza miundombinu, akatoa mfano wa ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi na ujenzi wa barabara nchi nzima, ambao mafanikio yake yasingefikiwa bila mikopo.

Uhimilivu wa deni 
Pamoja na kuendelea kukopa na deni kuwa kubwa, Dk Mpango alisema Serikali hufanya tathimini ya kimataifa kuhusu uhimilivu wa deni kila mwaka ili kujiridhisha na mpaka sasa pamoja na deni hilo kuonekana kubwa kimataifa, Tanzania ina fursa ya kuendelea kukopa zaidi.

Tofauti na inavyoelezwa kila mara na wanasiasa ambao wamekuwa wakichukua deni la taifa na kugawanya kwa idadi ya watu, ili kupata fedha zinazodaiwa kwa kila Mtanzania ikiwemo mtoto aliyezaliwa leo, Dk Mpango alitoa vigezo ambavyo ni vya kimataifa kupima uhimilivu wa deni.

Vigezo hivyo vinavyotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni, ni tofauti na kigezo cha kugawanya deni kwa idadi ya watu ambacho ni cha kisiasa na hakitumiki popote duniani isipokuwa kwa wanasiasa wa Tanzania.

Kigezo cha kwanza cha kimataifa cha upimaji wa uhimilivu wa deni kwa mujibu wa Dk Mpango, ni uwiano kati ya deni la taifa na pato la taifa, ambapo kimataifa deni halipaswi kuzidi asilimia 50 ya pato la taifa na kwa Tanzania, deni lipo asilimia 19 tu ya pato hilo.

Kigezo cha pili kinachotumika kupima uhimilivu wa deni la taifa ni deni la taifa kwa uwiano wa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Kimataifa, deni la taifa halitakiwi kuzidi asilimia 200 ya mauzo ya nje na kwa Tanzania, deni la taifa ni sawa na asilimia 97 tu ya mauzo ya huduma na bidhaa nje ya nchi.

Kigezo cha tatu kinachotumiwa kimataifa kupima uhimilivu wa deni la taifa kwa mujibu wa Dk Mpango, ni uwiano wa deni la taifa na mapato ya ndani. Kwa sasa kimataifa deni la taifa linatakiwa lisizidi asilimia 300 ya mapato ya ndani na kwa Tanzania, deni hilo la taifa ni asilimia 145.3 tu ya mapato ya ndani.
==


Advertisement
Punguzo la Bei 20% msimu huu wa Idd.Agiza saa hii ya Automatic, na lipa mzigo ukifika majiji yote TanzaniaAdvertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )