Thursday, August 11, 2016

Afungwa jela miaka mitatu kwa kumuibia mkewe dhahabu

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu Hussein Janga kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa dhahabu zenye thamani ya Sh5 milioni mali ya mkewe, Saida Mwakitete.
 
Pia, mahakama hiyo imemtaka mshtakiwa huyo kumlipa mkewe Sh5 milioni ambazo ni thamani ya dhahabu aliyoiba.
 
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa alisema ameridhishwa na mashahidi watatu wa upande wa mashtaka waliotoa dhidi ya mshtakiwa huyo.
 
Alisema upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi watatu ambao wamethibitisha shtaka hilo pasi na kuacha shaka.
 
“Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa nimejiridhisha pasi na kuacha shaka hivyo mshtakiwa ninamtia hatiani kama alivyoshtakiwa,’’ alisema Hakimu Mkasiwa na kuongeza:

“Hivyo Mahakama imekuhukumu kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na kosa la kuiba seti moja ya dhahabu yenye ya Sh5 milioni.” 

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
 
Akijitetea kwa nini asihukumiwe kifungo hicho, Janga aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa madai kuwa hali yake ya kiafya siyo mzuri. Aliomba apewe kifungo cha nje.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Janga alitenda kosa hilo Oktoba 27, 2014 katika maeneo ya Upanga wilayani Ilala. Alidaiwa kuiba dhahabu ambayo ni cheni ya shingoni, cheni ya mkononi na hereni mali ya mkewe.
 
Inadaiwa kuwa wawili hao walidumu katika ndoa kwa mwezi mmoja.

Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )