Monday, October 17, 2016

Masauni Ashauri Kifungu Cha Umoja Wa Kitaifa Kifutwe Katika Katiba Ya Zanzibar Ya Mwaka 1984


Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameshauriwa kuondosha mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka mwaka 1984.

Ushauri huo umetolewa na Katibu  wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa kimataifa wa Kamati Maalum ya NEC, CCM Zanzibar,  Hamad Yussuf Masauni katika Majumuisho ya ziara yake ya kuimarisha uhai wa Chama huko katika Ukumbi wa Amani Mkoa wa Mjini, Unguja.

Alisema huu ndio wakati mwafaka wa kuondosha mfumo huo kwani hauna tija katika maendeleo ya nchi badala yake ukiachwa itakuwa ni fursa kwa wapinzani kurudi tena katika serikali baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.

Alieleza kwamba nia ya CCM kukubali kuingia katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK) ni kushirikiana na vyama vya upinzani katika mipango ya maendeleo ya nchi pamoja na kumaliza siasa za chuki, hali ambayo CUF haikutaka kubadilika hivyo hakuna haja ya kubakisha mfumo huo katika Katiba ya Zanzibar.

Masauni aliwasihi Wawakilishi wa CCM kuhakikisha wanalinda kwa vitendo  maslahi ya Chama kwa kuandaa taratibu zote za kisheria kwa kufuta kipengele ndani ya Katiba kinachoeleza uwepo wa mfumo huo.

Alisema hatua ya mwisho itakuwa kurudi kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya kukubali ama kukataa kuendelea na SUK, jambo ambalo kwa sasa ni rahisi kwani wananchi wengi hasa wafuasi wa CCM hawataki kuendelea na serikali hiyo.

“ Huu ni wakati mwafaka wa kuifuta CUF katika siasa za Zanzibar kwani hatuwezi kuendelea kuwa na ushirikiano na Chama kinachojali maslahi binafsi pamoja sera za utengano badala ya kuwaunganisha wananchi.

Hakuna haja ya kuendelea na SUK kwani katika miaka mitano ya mfumo huo wenzetu walionyesha udhaifu mkubwa na kupelekea nchi kuanza kuyumba kwani hata viongozi wao wa majimbo hawakufanya chochote kwa wananchi na mzigo wote waliwasukumia viongozi wa CCM.”, alisema Masauni na kuongeza kuwa serikali iliyopo sasa inaendelea kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi.

Aliwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa juhudi zao za kufanya mabadiliko ya baadhi ya sheria ndani ya Katiba ya Zanzibar zilizokuwa zikiwajengea ngome ya kujiamini chama cha CUF katika Baraza hilo.

Akizungumzia Uchaguzi wa ndani ya CCM unaotarajiwa kufanyika mwaka 2017, Masauni alikemea tabia na vitendo vya kuendekeza siasa za makundi ndani ya CCM kwani  hali hiyo aliitaja kuwa  inasababisha kupatikana kwa viongozi wasiokuwa waadilifu ndani ya chama hicho.

Alisema baadhi ya viongozi wa CCM wanatakiwa kuwakataa watu watakaoingia ndani ya Chama hicho kuwania nafasi za uongozi kupitia nguvu za fedha na umaarufu kwani watu hao ndiyo chanzo cha kujengeka makundi yasiyokuwa na lazima ndani ya chama chetu.

“ Sote tunakumbuka athari mbaya ya makundi iliyojitokeza katika chaguzi zilizopita na kuendelea kutusumbua mpaka sasa kwani kuna baadhi ya wanachama waliweka mbele maslahi ya watu binafsi badala ya CCM.”, alifafanua Masauni.

Masauni ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, alieleza kwamba serikali haitovumilia kuona vitendo vya uhalifu vinaendelea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, na wanaofanya vitendo hivyo waache kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kupunguza kesi za uhalifu unaotokea katika maeneo mbali mbali nchini kwani kuna baadhi ya wananchi wanakataa kutoa ushahidi kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.

Mapema akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Bora afya Silima Juma aliwapongeza baadhi ya viongozi wa Majimbo wanaotekeleza vizuri Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi.

Alisema tokea kumalizika kwa Uchaguzi wa Marudio hali ya kisiasa ndani ya Mkoa huo imeimarika kwani kila mwanachama na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakifanya kazi za kujitafutia kipato bila ya usumbufu.

Nao wanachama wa Chama hicho, waliahidi kutoa ushirikiano kwa mambo mbali mbali yatakayoiwezesha CCM kurudi madarakani katika uchaguzi Mkuu ujao.

Walipongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi mbali mbali walizoahidi wananchi katika kampeni za Uchaguzi uliopita.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )