Monday, January 30, 2017

Daktari Aandika Barua ya Kuacha Kazi Baada ya Mkuu wa Mkoa Kumuweka Rumande Kwa Kosa la Kipindupindu

Mganga  Mkuu wa Wilaya ya Singida Vijijini, Dk. Erick Bakuza ameandika barua ya kuacha kazi

Dk. Bakuza amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache tangu alipopewa adhabu ya kuwekwa mahabusu na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi.

Dk. Nchimbi alitoa amri ya kukamatwa kwa daktari huyo kutokana na kuzuka ugonjwa wa kipindupindu ambao ulisababisha vifo vya watu wawili mwishoni mwa mwaka jana.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rashid Mandoa jana alithibitisha kuacha kazi kwa Dk. Bakuza.

“Ni kweli amewasilisha barua ya kuacha kazi lakini ninavyojua mimi si kweli kwamba ameacha kazi kutokana na adhabu aliyopewa na Mkuu wa Mkoa ya kuwekwa ndani.

“Kwanza ujue hakuwekwa ndani, na ameamua kuacha kazi kwa sababu amepata sehemu nyingine ambayo anaona ina maslahi anayohitaji yeye,” alisema.

Juhudi za kumpata Dk. Bakuza kuzungumzia hatua yake hiyo hazikuzaa matunda.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Wakati Mkurugenzi huyo akisema kwamba Dk. Bakuza hakuwekwa ndani, Mkuu wa Mkoa huyo, Dk. Nchimbi alithibitisha kwamba aliwekwa ndani kwa   saa tatu.

“Mimi nilitoa amri ya kukamatwa Daktari huyu na aliwekwa chini ya ulinzi kwa saa tatu.Nilimuweka ndani kwa sababu ya mazingira ambayo niliyakuta nilipokuja kuanza kuitumikia nafasi niliyoteuliwa ya ukuu wa mkoa, na nitatetea uamuzi wangu huo.

“Niliamuru akamatwe kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, kesi ya kwanza ya kuwapo kwa mgonjwa wa kipindupindu iliripotiwa Novemba 26, mwaka jana.

“Utaratibu unajulikana wazi kwamba ikifika kesi tano DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) anatakiwa atoe taarifa kwa MRO (Mganga Mkuu wa Mkoa).

“Desemba 4   hakutoa taarifa, ilipofika Desemba 16 vikatokea vifo viwili hakutoa taarifa hadi Desemba 18 ndipo akatangaza.

“Nikaona hakuwa makini katika kazi yake kwa sababu alipaswa kutangaza mapema ili tuchukue hatua za kudhibiti ugonjwa huo na naamini hata hivyo vifo visingetokea,” alisema.

Dk. Nchimbi alisema suala la kipindupindu halipaswi kuchukuliwa kisiasa na kwamba lenyewe lipo kitaalamu zaidi.

“Kuna taratibu ambazo hufuatwa lazima tupate evidence ya kutosha, watu wachukuliwe vipimo, yeye alinyamaza kimya. Wataalamu walipokwenda kuchunguza wakagundua kuna kipindupindu kwenye wilaya yake,” alisema.

Aliongeza: “Kwa hali hiyo niliona hakuwa makini katika kazi yake, hivyo nilitaka kumshtua tu awe makini, hakuwa makini.

“Katika hali ya kawaida angesema mapema tungechukua hatua mapema, tungetibu maji, tungesafisha visima na hata vifo visingetokea,” alisema.

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )