Friday, March 3, 2017

Hatima ya dhamana ya Godbless Lema Kujulikana Leo

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha leo inatarajiwa kusikiliza maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye amekuwa akiisaka kwa miezi minne sasa.

Mbunge huyo ambaye amekamatwa tangu Novemba 2 mwaka jana akiwa bungeni Dodoma, amewekwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, Arusha.

Jaji Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa hiyo namba 126 ya mwaka jana ambayo iliwasilishwa na mawakili wanaomtetea, Kibatala, John Mallya na Sheck Mfinanga.

Maombi hayo yanatokana na mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na Serikali mara baada ya uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka jana na Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha kumpa dhamana katika kesi inayomkabili ya kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Hata hivyo, Lema alikwama baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha kusudio la kukata rufaa. Mawakili wa Lema waliwasilisha Mahakama Kuu, maombi ya kutaka mapitio ya kesi hiyo, lakini yalitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi kutokana na upungufu na kutakiwa kukata rufaa.

Walifanya hivyo Desemba 2 mwaka jana lakini maombi yao yalitupwa kutokana na mapingamizi ya mawakili wa Serikali.

Waliomba kuongezewa muda wa kukata rufaa na Desemba 20 mwaka jana na Jaji Modesta Opiyo alikubali maombi hayo na kutupa mapingamizi ya Serikali.

Hata hivyo, siku ambayo ilipangwa Jaji Maghimbi kutoa uamuzi juu ya rufaa hiyo Jamhuri iliwasilisha notisi ya kupinga kusikilizwa.

Jaji Magimbi alisema kutokana na hilo, rufaa nyingine zitasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Februari 27, mapingamizi yote ya Jamhuri yalitupwa na Mahakama ya Rufaa, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa mapingamizi hayo.

Majaji waliotupa mapingamizi hayo ni Bernard Luanda, Kipenka Mussa na Stela Mugasha ambao walieleza kusikitishwa na mwenendo wa kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, Lema anatuhumiwa kuwa kati ya Oktoba 23 hadi 26 mwaka jana alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais Magufuli katika maeneo tofauti katika mikutano yake ya hadhara.

Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )