Tuesday, March 28, 2017

Malawi Yaichokonoa Tena Tanzania Kuhusu Ziwa Nyasa

Rais wa Malawi, Peter Mutharika ameanza tena chokochoko baada ya kutangaza kuwa hakuna nchi ambayo inamiliki kwa pamoja Ziwa Nyasa na kwamba haijafikia makubaliano na nchi yoyote, hivyo ameahidi kulinda umiliki na masilahi yake.

Kauli hiyo ni tofauti na mazungumzo ya Mutharika na Rais John Magufuli yaliyofanyika Januari 30 jijini Addis Ababa, Ethiopia wakati walipokuwa wakihudhuria kikao cha Umoja wa Afrika (AU).

Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Rais baada ya kikao hicho, ilisema marais wote wameridhishwa na jitihada zinazofanywa na jopo la usuluhishi lililoteuliwa na Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).

Jopo hilo linaongozwa na rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mindi Kasiga amekiri kuiona taarifa hiyo na alisema anayeweza kulizungumzia suala hilo ni Naibu Waziri.

“Tumeiona hiyo taarifa ila jaribu kumtafuta Naibu Waziri maana Waziri atakuwa nje ya nchi. Ninachofahamu baraza la usuluhishi bado linaendelea na vikao vyake. Ukimpata naibu waziri atakuwa na maelezo ya kina.”alisema Mindi.

Lakini, akihudhuria Siku ya Maji Duniani Jumatano iliyopita mjini Mangoshi, Rais Mutharika alisisitiza msimamo wa Malawi kulinda umiliki wa ziwa hilo dhidi ya watu aliowaita wavamizi.

Mutharika alisema Malawi ndiye mmiliki pekee wa Ziwa Malawi, ambalo huku linajulikana kama Ziwa Nyasa, na kuonya kuwa utawala wake hautavumilia watu watakaokuwa na nia ya kuyumbisha taarifa za umiliki.

“Hebu tulilinde ziwa letu. Hili ni ziwa letu na ninaposema ziwa letu namaanisha ziwa lote. Mtu yeyote asifanye kosa la kubadili umiliki ambao umekuwepo kwa miaka 124 iliyopita,” alisema Mutharika akikaririwa na tovuti ya Nyasa Times ya Malawi juzi wakati wa mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Nkopola Lakeshore mjini Mangochi.

“Tunathamini ziwa letu na tutahakikisha tunachukua hatua za kulilinda kwa gharama zozote,” alisema.

Mutharika aliwataka wananchi kupunguza matumizi mabaya ya maji ili yapatikane kwa ajili ya kilimo na viwandani wakati wa msimu wa ukame.

Hivi karibuni, Malawi na Tanzania zimejikuta katika mzozo wa umiliki wa Ziwa Nyasa lililo kusini mwa Tanzania, mzozo ambao umesababisha kuanza kwa mazungumzo ya usuluhishi kumaliza kutokubaliana huko baada ya nchi hizo mbili kushindwa kufikia muafaka. Mzozo wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa umekuwepo tangu mwaka 1967.

Lakini, mzozo wa hivi karibuni umeibuka baada ya Malawi kuanza utafiti wa mafuta na gesi kwenye ziwa hilo.

Hata hivyo, Mutharika alisema uchimbaji mafuta utaendelea katika ziwa hilo licha ya wanaharakati wa mazingira kuitaka Malawi iache mpango huo.

“Wale wanaohofia kuhusu mipango yetu ya kutafuta na kuchimba mafuta hawana sababu ya kuhofia. Kama tutaamua kuchimba mafuta katika ziwa, tutahakikisha tunatumia teknolojia safi,” alisema akikaririwa na Nyasa Times.
Advertisement
tang
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )