Monday, March 13, 2017

Rais Magufuli Atuma Salamu Za Rambi Rambi Kufuatia Kifo Cha Balozi Sir George Kahama ( mmoja wa Waasisi wa Taifa)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa Waasisi wa Taifa na Waziri Mstaafu Bw. George Kahama kufuatia kifo cha kiongozi huyo kilichotokea  tarehe 12 Machi, 2017.

Bw. George Kahama amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika Salamu zake Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru, maendeleo na ustawi wa jamii ya watanzania akiwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi hususani kuwa miongoni mwa Mawaziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri ambapo alishika wadhifa huo kwa awamu tatu za uongozi wa Tanzania.

“Sir George Kahama alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo, mwanasiasa mahiri, aliyewapenda Watanzania na aliyejitoa kushirikiana na viongozi wenzake akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere kupigania uhuru, kujenga misingi ya Taifa likiwemo Azimio la Arusha, kujenga misingi ya uchumi wa ujamaa na kujitegemea na mengine mengi, kwa hakika hatutamsahau”

“Japo kuwa Sir. George Kahama ametangulia mbele za haki, sisi viongozi tuliopo tutamuenzi kwa kuhakikisha tunaendeleza juhudi za kuipigania Tanzania aliyoshiriki kuijenga, na pia tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli katika salamu hizo.

Pamoja na familia ya Marehemu Bw. George Kahama, Mhe. Dkt. Magufuli amewapa pole nyingi wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wabunge, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma

==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )