Friday, June 30, 2017

Kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe Kuhusu Mauaji ya Watu Huko Kibiti

Mwenyekiti wa CHADEMA na Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe ameonesha kusikitishwa na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia yanayoendelea katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia msimamo wa CHADEMA juu ya mauaji hayo ambapo alisema chama hicho kinapingana na kinachotokea Mkoa wa Pwani.

“Kinachoendelea Mkuranga, Kibiti na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ni kitu kibaya. Hatuungi mkono mauaji ya raia na viongozi.

"Hilo naomba niliweke wazi, sisi kama chama hatuungi mkono mauaji ya viongozi bila kujali wanatoka chama gani au bila kujali wanatoka Serikali ipi au wana wajibu gani wala raia yeyote wa nchi yetu. Hatuungi mkono na tunalaani sana mauaji yanayoendelea.”

Aidha, alisema wanasikitika na namna Serikali inavyolichukulia suala hilo akiwataka viongozi wa kisiasa kuviachia vyombo vya Ulinzi na Usalama vifanye kazi yake.

“Tunasikitika na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyoshughulika na jambo hili. 

"Kauli za viongozi wetu mbalimbali za majigambo zinaonekana kuwachochea wauaji kwa sababu linapotoka tamko lolote la majigambo anakufa mtu usiku ama anakufa mtu kesho yake. 

"Viongozi wetu wa kisiasa waachie vyombo vya Ulinzi na Usalama vifanya kazi. Matamko mengi yanatolewa na viongozi wetu wa kisiasa. Hatuna hakika ni nini kinaendelea.”

Katika kutafuta suluhisho zaidi juu ya tatizo la mauaji ya Pwani, Mbowe alivitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutumia ujuzi wa ziada kukabiliana na wauaji ikiwa pia kuwashirikisha watu mbalimbali na taasisi mbalimbili.

“Tunataka Majeshi yetu na vyombo vyetu vya Ulinzi na Ulasama vitumie weledi wa ziada. Sio kila wakati nguvu tu inaweza ikasaidia. Busara nyingine zote zitumike; Wazee watumike, Vyombo vya Serikali vitumike, Viongozi wa Kidini watumike.”
Advertisement
tang
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )