Monday, June 12, 2017

Profesa Muhongo Kitanzini Tena.....Ni Baada ya Rais Magufuli Kuviagiza Vyombo vya Dola Vimuhoji Kwa Kusaini Mikataba Mibovu ya Madini

Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt Magufuli ameagiza viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini, Manaibu wake, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Maafisa wa TRA, na watumishi wengine waliohusika katika upotevu wa matrilioni ya fedha kupitia sekta ya madini wahojiwe.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu alipokuwa akipokea ripoti ya pili ya kamati iliyokuwa ikichunguza makinikia yaliyopo kwenye makontena bandarini iliyoundwa na wanasheria ya wachumi.

Akizungumza kwa uchungu, Rais Magufuli alisema kuwa Tanzania imejaliwa na kila aina ya madini ambayo unaweza kuyataja hadi ukasahau lakini bado sisi ni maskini. 

Akitaja baadhi ya madini alisema kuna dhahabu, almasi, tanzanite, gesi za kila aina na vitu vingine mbalimbali lakini tumebaki masikini kutokana na viongozi kutokuwa wazalendo.

Akisoma ripoti hiyo Ikulu leo, Mwenyekiti wa Kamati, Prof. Nehemiah Osoro alisema kuwa Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini wa kipindi kilichopita walisaini mikataba ya madini ambayo haikuwa na faida kwa taifa na hivyo kusababisha nchi kupoteza mapato kwa kutoa misamaha ya tozo mbalimbali.

Prof. Osoro alieleza zaidi kuwa kwa kutumia mamlaka aliyonayo, Mawaziri waliopita wamekuwa wakiwaongezea muda wa kufanyakazi au eneo la uchimbaji makampuni ya madini bila kufuata sheria. Akitolea mfano hapa, Prof. Osoro alisema kuwa, Waziri Prof. Muhongo alifanya hivyo kwa mgodi wa North Mara.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kipindi cha mwisho cha Rais Mkapa, Daniel Yona amewahi kushtakiwa kwa kosa la kuongezea  mkataba  wa  ukaguzi  wa  madini  kampuni MS  ALEX  STUWART  kwa  miaka  miwili zaidi  kuanzia  tarehe  14 Juni 2005  hadi  tarehe  23 Juni 2007 bila kufuata utaratibu.

Rais ameagiza viongozi hao wahojiwe ili waeleze kwanini walifanya waliyoyafanya na kwa manufaa ya nani kitu kilichopelekea taifa kupoteza fedha nyingi.

Miongoni mwa watakaohojiwa kufuatua amri hii ya Rais ni, William Ngeleja, Prof. Sospeter Muhongo, Nazir Karamagi, Daniel Yona, Andrew Chenge, Fredrick Werema, Johnson Mwanyika.
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )