Loading...

Sunday, September 24, 2017

Tundu Lissu Aikataza Familia Kuandika Barua ya Matibabu Serikalini

Familia ya mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, imesema imezuiliwa kuandika barua kwa ajili ya kuiomba serikali kugharamia matibabu ya mbunge huyo kwa madai amehaidi suala hilo atakuja kulishughulikia yeye mwenyewe hivi karibuni.

Hayo amebainisha kaka wa mbunge huyo ambaye pia ni msemaji wa familia, Alute Mughwai baada ya kupita siku kadhaa tokea serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kutoa kauli yao ya kusema mgonjwa ni mbunge ambaye anayehitaji matibabu zaidi lakini kwa kuwa yupo nje ya utaratibu wa serikali na ili serikali iweze kushiriki ni lazima yawepo maombi ya kufanya hivyo.

"Majira ya saa nne hivi niliweza kuzungumza na Mhe. Tundu Lissu akiwa hospitalini Nairobi baada ya kumjulia hali nilimueleza taarifa ya Mhe. Waziri kwamba tuandike barua ili aweze kupata matibabu kwa gharama za serikali, akanijibu kuwa jambo hilo atalizungumzia yeye mwenyewe siku za hivi karibuni. Kwa sababu yeye anaamini ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anahaki zote anazostahili kulipwa, kama mbunge ikiwa ni pamoja na kupatiwa matibabu endapo ataugua au atapatwa na maradhi", amesema Alute.

Pamoja na hayo, kaka wa Lissu ameendelea kwa kusema "Mpaka hivi sasa jeshi letu la polisi halijaweza kumkamata mshtakiwa yeyote juu ya tukio la Lissu wakati jambo hilo lilitokea mchana kweupe na watu wengi walishuhudia. Sasa mazingira hayo yametupa wasiwasi kama tukio hilo litachunguzwa kikamilifu, hatuna wasiwasi na uwezo wa polisi wetu kufanya huo uchunguzi lakini shida yetu ni utayari".

Aidha, Alute amesema wameshamuandikia barua Mwanasheria Mkuu wa serikali ili waweze kupatiwa msaada wa kiuchunguzi zaidi dhidi ya tukio hilo lililomtokea ndugu yake.

"Barua tumeandika Septemba 16, mwaka huu kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali maana ndiyo mamlaka inayopaswa kuchukua hatua za kuombwa msaada wa kiupelelezi kwa niaba ya serikali yetu huko nje ya nchi, na hiyo barua nimeinakili kwa Mhe. Waziri Sheria na Mambo ya Katiba", amesisitiza Alute.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa na risasi nje ya nyumba yake mjini Dodoma wakati akitokea Bungeni na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 na mwishowe kukimbiziwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )