Friday, October 6, 2017

Aga Khan kutua nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli

Kiongozi wa madhehebu ya Ismailia duniani, Mtukufu Aga Khan anatarajia kutembelea Tanzania Oktoba 11 na 12 kwa mwaliko wa Rais John Magufuli.

Mtukufu Aga Khan atawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa nne asubuhi akitokea Uganda atakakokwenda kuhudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni.

Akizungumzia ziara hiyo leo Ijumaa, Ofisa Mawasiliano wa Baraza la Aga Khan, Shelmina Shivji amesema ziara hiyo itafungua fursa katika sekta mbalimbali na kukuza uchumi wa Taifa.

Amesema mwaliko huo wa Rais Magufuli unaonyesha uhusiano mzuri kati ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) na Serikali ya Tanzania.

"Mtukufu Aga Khan amekubali mwaliko wa Rais Magufuli na katika ziara yake ya siku mbili nchini atakuwa na mazungumzo na Rais na kukutana na watendaji wa AKDN," amesema.

Shivji amesema Mtukufu Aga Khan ni mwekezaji mkubwa nchini katika sekta za afya, elimu, kilimo na maendeleo ya jamii.

Mratibu wa mawasiliano ya jamii ya Ismailia, Khan Ramji amesema maandalizi ya mapokezi ya kiongozi huyo yanaendelea vizuri kwa upande wa Serikali na Jumuiya ya Ismailia.

"Wananchi wajitokeze kwa wingi uwanja wa ndege wa JNIA kumpokea Mtukufu Aga Khan ambaye anatarajiwa kufika saa nne  asubuhi," amesema Ramji.

Julai 11, Jumuiya ya Waismailia nchini iliungana na wenzao duniani kuadhimisha miaka 60 ya uongozi wa Aga Khan ambaye ni Imamu wa 49 wa jumuiya hiyo.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )