Friday, October 27, 2017

Kigwangalla asitisha operesheni ya kuchoma makazi Loliondo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla leo Ijumaa ametangaza kusitishwa operesheni zilizokuwa zinaendelea katika pori tengefu la Loliondo na ametaka mifugo yote inayoshikiliwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo haijafikishwa mahakamani kuachiwa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika mji wa Wasso Loliondo baada ya kukutana na kamati ya ulinzi na usalama na madiwani, Dk Kigwangalla amesema amechukua uamuzi huo ili kusimamia dhana na uhifadhi endelevu na shirikishi.

Amesema  wizara hiyo itaendelea kusimamia sheria za uhifadhi kwa kushirikiana na jamii na haitakubali watu wachache kuvunja sheria za uhifadhi.

"Kwa mamlaka niliyonayo kwa watendaji wote wa wizara walio chini yangu, natangaza kusitisha operesheni iliyokuwa inaendelea na kurejeshwa kwa wananchi mifugo yote iliyokuwa inashikiliwa na wahifadhi ambayo uamuzi wake, hausubiri Mahakama," amesema.

Waziri Kigwangalla pia aliagiza wataalam wa maji katika Halmashauri ya Ngorongoro, kushirikiana na wataalam wa hifadhi kutoa maeneo nje ya hifadhi ili mifugo ya wananchi ipate maji.

Hata hivyo, amesema ili kudhibiti mifugo ya nchi jirani, kuingia

katika maeneo ya hifadhi nchini, mifugo yote sasa inatakiwa kuwekwa alama na mifugo kutoka nje itakayokamatwa itataifishwa.

Waziri Kigwangalla amesema anataka mamlaka ambazo zipo chini yake, kurejea katika kazi ya msingi kuhifadhi na kupambana na ujangili badala ya kufanya kazi ya kuchunga mifugo inayokamatwa.

"Uchukuaji mifugo inawafilisi wananchi na inajenga uadui baina ya wahifadhi na wananchi...kuna mifugo inakamatwa inakaa muda mrefu katika hifadhi baadhi inakufa na mingine inachungwa hifadhini, jambo ambalo sio wajibu wa wahifadhi," amesema.

Akizungumzia mifugo mingine ya wananchi, iliyokamatwa maeneo mengine ya hifadhi nchini, Dk Kigwangalla alitoa siku saba kwa watendaji wa wizara yake kumpa mapendekezo ya namna bora ya kutatua tatizo hilo ili afanye maamuzi.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )