Thursday, October 12, 2017

Sheikh Issa Ponda Afunguka Walichoongea na Tundu Lissu Nairobi

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ameelezea jinsi mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anavyopanga mikakati ya kurejea katika siasa baada ya kupona.

Ponda amesema hayo baada ya kumtembelea Lissu aliyelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa baada ya kushambuliwa kwa takriban risasi 30 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake mjini Dodoma katika tukio lililotokea mchana Septemba 7.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar  ulioishia kwa baadhi ya waandishi wa habari kukamatwa na Jeshi la Polisi, Sheikh Ponda alisema safari yake ya Nairobi ilikuwa na malengo manne.

Aliyataja madhumuni hayo kuwa ni kumjulia hali Lissu, kumuombea dua na kumjengea matumaini ya afya yake, kumjengea matumaini endelevu ya harakati zake za umma na kujenga mazingira ya kutosha kuzungumzia tukio hili.

“Katika kipengele cha tatu, tulipokuwa tunapeana na kubadilishana hoja, nilipata hisia nzito kwake,” alisema Sheikh Ponda.

“Maana yeye aliye kitandani alinipa mimi matumaini makubwa. Alisema anaamini yuko karibu kurudi jukwaani na ataanzia pale atakapokuta kasi ya mabadiliko imefikia.

“Alinieleza kazi muhimu za kuwajenga watu anazofanya akiwa pale kitandani. Alinieleza anaamini damu yake na yangu na nyingine zitakazomwagika kwa namna hii, zitawafanya Watanzania kupata uhuru wa kweli wenye thamani.”

Sheikh Ponda alisema tukio hilo na mengine ambayo yamekuwa yakitokea nchini yawe funzo na kuifanya jamii kujenga umoja na ushirikiano katika kulirudisha Taifa katika njia sahihi.

“Izingatiwe kwamba ikiwa tatizo lipo na watu hawasemi kama lipo, basi litaendelea kuwepo na wasababishaji pia wataendelea kudumu,” alisema.

“Na wale wanaoamini hali iliyopo ni kwa Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake, tuunganishe nguvu kuhakikisha Serikali inatekeleza wajibu huo.

“Masheikh, maaskofu, mapadri, wana vyuo, viongozi wa upinzani na hata viongozi wazuri walioko CCM waiambie ukweli Serikali. Kimya chao ni hasara na kitawanyima hadhi ya anuwani yao.”

Sheikh Ponda alisema kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwapo na matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yanalichafua Taifa katika uso wa kimataifa.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni mauaji ya kutisha, maiti za watu kuokotwa kwa wingi na zinaendelea kuokotwa, raia na viongozi kadhaa wametekwa na kupotea, viongozi mashuhuri wa vyama vya siasa vya upinzani na wa taasisi za kidini wanashambuliwa kwa silaha nzito kwa lengo la kuuawa.

Alisema kwa kuwa roho za Watanzania hivi sasa ziko juu na baadhi wamepoteza matumaini ya usalama wao, ni jukumu la Serikali kuhakikisha usalama wa raia wake unakuwapo wakati wote.

Mara baada ya mkutano huo uliofanyikia Hoteli ya Iris iliyopo Mtaa wa Livingstone Kariakoo kumalizika, na waandishi kadhaa kuondoka, askari wa Jeshi la Polisi walifika kumfuata Sheikh Ponda.

Askari hao waliokuwa wamevalia kiraia na wengine sare, walikuwa kwenye gari mbili na kuzuia mtu yeyote kutoka huku wakitaka kujua alipo Sheikh Ponda na walipoelezwa kwamba ameshaondoka, walianza kumsaka.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )