Tuesday, November 14, 2017

Vyama vya siasa vyatakiwa kufanya kampeni kwa kuzingatia taratibu za uchaguzi

Hussein Makame-NEC
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistolces Kaijage amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili ya Uchaguzi.

Jaji Kaijage ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa NEC na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana Novemba 13 kuelekea Uchaguzi mdogo wa madiwani.

Alisema iwapo ukiukwaji au uvunjaji wa Maadili hayo utatokea, Chama au Mgombea awasilishe malalamiko hayo mbele ya Kamati husika ili ishughulikiwe kisheria.

Aliwakumbusha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 Tume inayo mamlaka ya kuruhusu kuwepo kwa Kampeni za Uchaguzi katika maeneo ya Uchaguzi na siyo Mikutano ya Vyama vya Siasa.

Hivyo, kampeni hizo zifanyike kwenye Kata husika na inategemewa kuwa Mikutano ya Kampeni italenga kuwashawishi, kwa namna ya kistaarabu, wananchi wa Kata husika ili wamchague Mgombea anayefanyiwa kampeni.

”Kwa mujibu wa kipengele cha 2.1. (c) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 tunategemea kila Chama cha Siasa kiendelee kufanya Kampeni kwa mujibu wa ratiba. Kampeni zote zinatakiwa kuanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni,” alisema Jaji Kaijage.

Aliongeza kuwa kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Tume imekwisha kutoa ushauri kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya ili katika kipindi hiki cha Uchaguzi wahakikishe wanazingatia wajibu wao na ukomo wa madaraka yao katika shughuli za Uchaguzi kuanzia kipindi cha Kampeni hadi kutangazwa kwa Matokeo.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi kailima Ramadhani aliaviomba Vyama vya Siasa kuwahimiza wanachama na wapenzi wao walioandikishwa kuwa Wapiga Kura wajitokeze Siku ya Uchaguzi kwenda Kupiga Kura zao bila hofu yoyote kuhusu usalama wao.

“Ni imani ya Tume kuwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mtakuwa chachu ya kuwaongoza na kuwaelekeza wanachama, wafuasi na mashabiki wenu katika kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu,” alisema Kailima.

Uchaguzi Mdogo wa madiwani katika kata 43 za Tanzania Bara, unatarajiwa kufanyika tarehe 26 Novemba, 2017 ambapo wapiga kura 333,309 wanategemewa kupiga kura siku ya uchaguzi huo.


Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )