Loading...

Saturday, December 23, 2017

Ndugai akosoa upangaji vituo vya kazi kwa walimu

Spika wa Bunge, Job Ndugai amepinga mpango wa Serikali wa kuwapangia vituo vya kazi moja kwa moja walimu wanaoajiriwa, akihoji ni kwa nini inapoka madaraka ya halmashauri.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 23,2017 ikiwa ni siku moja baada Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo kutangaza majina ya walimu 3,033 waliopangiwa vituo vya kazi.

Katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Dodoma leo, Spika Ndugai amehoji Tamisemi ni nani hata aweze kujua ikama ya walimu shuleni. Amesema wamekuwa wakijaza walimu maeneo yasiyo na mahitaji.

"Hili jambo linakera, yaani kila mahali sasa ni Tamisemi hadi napata shaka sasa, hivi hii zana ya D by D (ugatuaji wa madaraka) ina maana haijatafsiriwa vyema au ndiyo kupoka madaraka kwa wengine," alihoji Ndugai.

Spika ametoa mfano wa Shule ya Banyibanyi wilayani Kongwa ambayo amesema ina wanafunzi wanaoingia kidato cha tatu lakini hawajawahi kusoma masomo ya sayansi hata siku moja.

"Lakini juzi hapa mmepanga walimu na nilipita tena hapo hakuna hata mwalimu. Hawajasoma hesabu, fizikia, baiolojia, kemia na jiografia; nauliza tena wanasema Tamisemi, hivi hao walisoma wapi na ninyi mmesoma shule zipi," alihoji.

Ndugai amewatupia mzigo wabunge wa Mkoa wa Dodoma amesema wanatakiwa kuupinga mpango huo bungeni wakati yeye akiongoza vikao vya Bunge.

Pia, amepinga mpango wa utoaji fedha kwa vikundi amesema umepitwa na wakati kwa kuwa zinaliwa bure.

Amesema hakuna umuhimu wa kusema watu waunde vikundi ndipo wapewe fedha au uwezeshwaji, badala yake waangaliwe mtu mmoja mmoja ambao wanakuwa na uwezo wa kuzalisha na kisha wafuatiliwe.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe kwa nyakati tofauti waliunga mkono hoja ya kutopeleka fedha kwa vikundi.

Lusinde amesema kumekuwa na utitiri wa vikundi baada ya kusikia kuna fedha wakati uwezo wa uzalishaji haupo.

"Namuunga mkono Spika katika hili, tunaunganisha watu hata wasiokuwa na mbinu za uzalishaji, naomba tuachane na vikundi havina tija kwa kuwa wanagawana fedha tu," amesema Lusinde.

Profesa Mwamfupe amesema Serikali inagawa vibaya rasilimali fedha kwa kauli ya kasungura kadogo tugawane lakini zinaishia kutoleta tija.

Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewaagiza wakurugenzi wa wilaya kuangalia ikama ya walimu na kuwatawanya mara moja.

Kuhusu fedha za vikundi kwa vijana na akina mama amesema jambo hilo liko kisheria. Amesema hakuna ubaya kuwasaidia watu mmoja mmoja ambao wanajiweza katika uzalishaji.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )