Saturday, December 30, 2017

Serikali yawatoa hofu wananchi kuhusu deni la Taifa

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imewatoa hofu wananchi kuhusu uvumi wa kuongezeka kwa deni la Taifa kwamba deni hilo ni himilivu na liko chini ya ukomo wa hatari.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam  na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philipo Mpango wakati akitoa mwenendo wa  hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti  ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.

Dkt. Mpango alisema kuwa katika tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka huu inaonesha kuwa uwiano wa deni hilo na pato la Taifa ni asilimia 32.5 likilinganishwa na ukomo wa asilimia 56.

“Katika kuangalia ukomo wa deni hili ambao uko chini, inaonesha kuwa deni hili ni himilivu  katika kipindi cha muda wa kati na muda mrefu,” alisema Dkt. Mpango.

Akieleza takwimu hizo, Waziri Mpango amesema kuwa mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 47,823.1 ikilinganishwa na bilioni 42,552.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2016 ambapo kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 13,417.5 ni deni la ndani sawa na asilimia 28.1 na shilingi bilioni 34,405.6 ni deni la nje ambalo ni sawa na asilimia 71.9.

Dkt. Mpango alisisitiza kuwa ongezeko hilo lilitokana na kupatikana kwa mikopo mipya ya nje na ndani ya nchi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maeneeleo.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa mradi wa umeme Kiwira (Kiwira Coal Mine), miradi ya uboreshaji wa huduma za maji kwa jamii, mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kinyerezi na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege ambapo miradi hiyo  itawezesha watanzania kufika uchumi wa kati wenye viwanda.

“Mambo muhimu ya kujiridhisha nayo ni kwamba mikopo inayokopwa itumike katika kujenga uwezo zaidi wa kuzalisha mali na huduma nzuri kwa watanzania,” alisisitiza Dkt. Mpango.

Aidha Waziri Mpango amesema kuwa kufuatia hatua zinazochukuliwa na Serikali, ukwasi kwenye benki za biashara uliongezeka na kusaidia kupungua kwa riba ya mikopo baina ya mabenki na kufikia wastani wa asilimia 3.53 mwezi Novemba mwaka huu kutoka wastani wa asilimia  14.93 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2016/2017.

Vilevile riba za dhamana za Serikali zilishuka kutoka wastani wa asilimia 15.56 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016/2017 hadi asilimia 8.76 mwezi Novemba, 2017 na kuongeza kuwa Serikali inatarajia kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi itaanza kuimarika.

Aidha, Dkt. Mpango amewaonya watu wanaotoa takwimu za uongo kuacha mara moja kwani wanaipotosha jamii, huku akiwataka waandishi wa habari kupata takwimu maalumu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ili kuweka takwimu sahihi.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )