Saturday, December 9, 2017

Wabunge wa CHADEMA waachiwa kwa dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imetupilia mbali hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya wabunge Suzan Kiwanga(Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombero) na washtakiwa wengine 37 waliofikishwa mahakamani hapo kwa makosa nane.

Mbele ya Hakimu, Ivan Msaki mahakama ilitupilia mbali kiapo hicho na kueleza kuwa washtakiwa wote dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya Sh 5 milioni na pia barua za dhamana lazima zisainiwe na wenyeviti wa vijiji ama maofisa watendaji.

Katika kiapo kilichowasilishwa awali mahakamani hapo na upande wa mashtaka kupitia wanasheria wa Serikali, Sunday Hyera na Edga Bantulaki ulieleza sababu walizodai kuwa ni za msingi za kupinga dhamana na kwamba kuwepo nje kwa washtakiwa  kunaweza kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.

Kufuatia hoja hiyo upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili wanne wakiongozwa na wakili Peter Kibatala uliamua kuwasilisha hati ya kupinga kiapo hicho kwa madai kuwa  kiliandikwa bila ya kuzingatia misingi na matakwa ya kisheria.

Wakili Kibatala alidai kuwa miongoni mwa mapungufu yaliyokuwemo kwenye kiapo hicho ni pamoja na kutokuonyesha majina ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Malinyi (OCD) ambaye alitajwa kwenye kiapo hicho kama chanzo kilichotoa taarifa zilizotengeneza mashtaka yanayowakabili wabunge hao na wenzao.

Alidai kuwa mapungufu mengine yaliyokuwepo kwenye kiapo hicho ni utofauti wa tarehe ya kuandika kiapo hicho na kusainiwa na hivyo waliiomba mahakama kuzingatia mapungufu hayo.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria baina ya pande hizo mbili Hakimu Msaki aliamua kupitia hoja za msingi za kisheria na hivyo kubaini mapungufu yaliyopo kwenye kiapo hicho na kueleza kuwa mapungufu hayo hayawezi kurekebishwa na kwamba kazi ya mahakama ni kutafsiri sheria na si kufundisha namna ya kuandika kiapo.

Kwa msingi huo Hakimu Msaki alitupilia mbali hati hiyo ya kiapo cha kupinga dhamana na kueleza kuwa washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana wakati kesi yao ikiendelea.

Kabla ya kupewa dhamana washtakiwa hao walikaa rumande kwa siku 12 hali iliyosababisha kesi hiyo kuvuta hisia za watu hususani viongozi na wanachama Chadema waliokuwa wakifulika mahakamani hapo.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )