Loading...

Friday, February 9, 2018

Ugonjwa wa Aveva Wasababisha Kesi Kupigwa Kalenda

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, na makamu wake, Geofrey Nyange, ambao wanakabiliwa na shauri la utakatashaji wa fedha, kutokana na Aveva kuwa mgonjwa.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo ya kutakatisha Dola za Marekani 300,000 hadi Februari 22, mwaka huu.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa.

Swai alieleza Aveva ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa kwa ajili ya kutibiwa ugonjwa wa figo.

Alidai wamepata taarifa mshtakiwa ameshatoka hospitali,lakini ameshindwa kufikishwa mahakamani kwa sababu afya yake haijawa ya kuridhisha.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 22, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016 wakionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Ilidaiwa katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 jijini Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za Marekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Katika shtaka la nne, Aveva anadaiwa kati ya Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za Marekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano, Nyange anadaiwa Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )