Saturday, March 3, 2018

Kilichoendelea Mahakamani Katika Kesi ya Rugemariila wa ESCROW

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana iliipiga kalenda kesi inayomkabili mfanyabiashara James Rugemalila na mwenzake hadi Machi 16.

Rugemarila na mfanyabiashara Harbinger Sethi wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. bilioni 309.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leornad Swai alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na upande wa Jamhuri uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa tena Machi 16 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu. Walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Julai, mwaka huu upande wa Jamhuri ulidai:

Kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam Sethi na Rugemalira walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Ulidai katika shitaka la pili kati ya Oktoba 8,2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shitaka la tatu linalomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni na kuonyesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi kitalu namba 887, Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua sio kweli.

Pia, Sethi anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa nia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Kimaro alidai katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati, Kinondoni, na kwa vitendo vyao hivyo waliisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

pande wa Jamhuri ulidai kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 katika maeneo tofauti Dar es Salaam, kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Katika shitaka la nane, ulidai kuwa Novemba 29, 2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BOT, dola za Marekani milioni 22.1 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Aidha, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh. bilioni 309.4 kutoka BOT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao uhalifu.

Katika shitaka la 10, inadaiwa kuwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha ambazo ni Sh. bilioni 73.5 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Pia ilidaiwa kuwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi hilo, Rugemarila alitakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani 22,000,000 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Jamhuri pia ilidai Januari 28, 2014 katika tawi la Benki ya Stanbic wilaya ya Kinondoni Sethi alihamisha kwenda Afrika Kusini Rand 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land Rover Sandton ya Afrika Kusini wakati akijua katika kipindi anahamisha, fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Washitakiwa wapo rumande tangu Julai, mwaka jana kwa kuwa mashitaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )