Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Tuesday, May 8, 2018

Mahakama Yaubana Upande wa Mashitaka Kesi ya vigogo Uthamini wa madini ya almasi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili vigogo wawili wa uthamini wa madini ya almasi wa Serikali, kwamba kufikia Mei 21, 2018 watoe majibu sahihi kuhusu ulipofikia upelelezi wa kesi hiyo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbrad Mashauri ameeleza hayo jana Jumatatu Mei 7, 2018 muda mfupi baada ya wakili wa Serikali, Saada Mohammed kueleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Baada ya Saada kueleza hayo, wakili wa utetezi Nickson Ludovick alidai walitegemea upande wa mashtaka wangeiambia mahakama ni lini wataendelea na kesi hiyo kwa sababu walishasema upelelezi umekamilika.

Aliiomba mahakama imwamuru Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kueleza ni lini kesi itaendelea kwa sababu katika kumbukumbu za mahakama zilizopo, zinaonyesha kesi ilishakuwa tayari kwa kuanza kusikilizwa.

Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Elia Athanas alidai jalada bado linashughulikiwa katika sehemu ambazo hazipo sawa na hakuna uzembe wowote unaofanywa na ofisi ya DPP.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Mashauri aliamuru upande wa mashtaka Mei 21, 2018 kuja na majibu sahihi kuhusu hatua ya upelelezi ilipofikia.

Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo na mthamini almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Washtakiwa hao wanasota mahabusu kutokana na DPP kuzuia dhamana zao.

Kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )