Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Thursday, June 28, 2018

Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Waingilia Kati Sakata la Korosho

Baraza la uongozi la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) limetoa tamko kuhusu mjadala wa kisheria juu ya tozo ya ushuru wa korosho ghafi zinazouzwa nje ya nchi.

Katika tamko lililotolewa  jana Juni 27,  TLS imesema mwaka 1996 Bodi ya Korosho na Wadhamini wa Mfuko wa Kuendeleza Korosho waliingia makubaliano na Bodi ilikubali kuulipa mfuko asilimia mbili kati ya tatu ya ushuru wa korosho wanazolipa wauzaji wa korosho kwa mujibu wa Kanuni ya 21(1) ya Tangazo la Serikali namba 369 la mwaka 1996.

Baraza hilo limesema mwaka 1999, Bodi ilikuwa imeulipa mfuko Sh1.73 bilioni zilizokusanywa kutoka ushuru huo.

Kutokana na ukaguzi, mfuko uliishitaki Bodi ya Korosho kwa kushindwa kulipa Sh1.8 bilioni. Hukumu ya Rufaa ya shauri la madai namba 18 ya mwaka 2001 kati ya mfuko na bodi, Mahakama ya Rufaa Iliamua kuwa mfuko haukuwa na haki ya kulipwa asilimia mbili ya ushuru huo kwa sababu (a) bodi haikuwa wakala wa mfuko na (b) Kanuni 21(1) ya Gazeti la Serikali (GN) namba 369 haikuelekeza fedha hizo kupewa mfuko.

Sehemu ya 4 ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2010, Bunge lilirekebisha sheria ya korosho na marekebisho hayo yalielekeza kutozwa kwa ushuru wa korosho unaolipwa na wauzaji kwa asilimia 15 ya thamani ya mazao kabla ya kupakiwa kwenye meli au dola za Marekani 160 kwa tani moja ya korosho inayouzwa, au yoyote itakayokuwa kubwa.

TLS inasema Sheria ya Fedha ya Mwaka 2010 iliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi hiyo na kukabidhi asilimia 65 kwa mfuko wa kuendeleza zao la korosho.

“Kwa hiyo, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2010, inaitaka TRA kuwasilisha kwenye mfuko asilimia 65 ya ushuru wote wa korosho kutoka kwa wauzaji kuanzia Julai 21, 2010 mpaka hapo sheria tajwa itakapokuwa imebadilishwa au kufutwa,” inasema TLS katika taarifa iliyosainiwa na Rais wa chama hicho, Fatma Karume.

TLS inasema fedha iliyokusanywa na kutowasilishwa kwa mfuko ni suala la kisheria na kwamba, mfuko unaweza kufungua madai mahakamani kwa hoja hiyo.

TLS inasema shauri namba 18 la mwaka 2001 liliamuliwa kabla ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2010 na haina maana wala uzito wowote kwa mjadala unaoendelea katika jamii na vyombo vyake.

"Uamuzi wa shauri lile ulihusu tu mahusiano kati ya Bodi ya Korosho na Mfuko wa Korosho na tafsiri ya kanuni ya 21 (1) ya Gazeti la Serikali namba 369 ya mwaka 1996," linasema tamko hilo.

TLS inasema shauri la madai namba 18 la mwaka 2001 halikufuta sehemu ya 4 ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2010.

"Katika kuimarisha utawala wa sheria nchini, tunashauri watu wote walio kwenye mjadala huu kuheshimu sheria zilizopitishwa na Bunge mpaka hapo zitakaporekebishwa na Bunge au kufutwa na Mahakama.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )