Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Thursday, June 14, 2018

Mahakama yatengua kifungo cha miaka 15 jela cha Askari Polisi aliyemuua Mwangosi na kuamuru ashtakiwe upya

adv1
Mahakama ya Rufaa imetengua kutiwa hatiani kifungo cha miaka 15 jela alichopewa askari polisi, Pacificus Simon aliyeshtakiwa kwa kumuua mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na kuamuru ashtakiwe upya.

Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa, Bernard Luanda, Shaaban Lila na Rehema Mkuye katika kikao kilichofanyika mkoani Iringa Juni 4, limesema utaratibu wa usikilizwaji wa kesi ulikiukwa kwa jaji aliyetoa hukumu kutorekodi na kuwasomea wazee wa baraza majumuisho ya kesi hiyo ili watoe maoni kama sheria inavyotaka.

“Kwa kutumia mamlaka ya Mahakama hii kama ilivyowekwa chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufaa (Aja), tunatamka kuwa mwenendo wote wa kesi na hukumu ni batili. Tunafuta hatia na kuamuru mrufani ashtakiwe upya mbele ya jaji mwingine na wazee wapya wa baraza,” inasema hukumu ya majaji hao.

Majaji hao walisema kabla ya kuanza kusikiliza rufaa, walibaini upungufu wa kisheria kuhusu mwenendo wa usikilizaji wa kesi.

Kifungu cha 298 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinatamka wazi pindi pande mbili zinapofunga kesi, jaji atatakiwa kutoa majumuisho ya ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi, na kuwataka wazee watoe maoni yao kuhusu kesi na kurekodi mwenendo huo kwa maandishi.

Majaji hao wamesema katika kesi hiyo inaonekana majumuisho yalifanywa kwa mdomo.

“Kama yalifanywa kwa mdomo tutajuaje kama jaji alifanya majumuisho ya kesi hiyo sawasawa na kama inavyotakiwa na sheria?” wanahoji katika hukumu hiyo.

Hukumu inasema, “Ni pale tu majumuisho ya kesi yanapokuwa katika maandishi tunaweza kuona kwa mfano, wazee wa baraza walijulishwa mambo yanayounda kosa la kuua, nani ana jukumu la kuthibitisha na kwa kiwango gani.”

Majaji wanasema kushindwa kuonyesha majumuisho ya kesi kwa wazee wa baraza kwa maandishi kumebatilisha mwenendo mzima wa kesi.

Julai 2016, Mahakama Kuu ilimhukumu kwenda jela miaka 15 askari Simon baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Mwangosi bila kukusudia.

Mwandishi huyo aliuawa Septemba 2, 2012 eneo la Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa baada ya kutokea kutoelewana kati ya wafuasi wa Chadema na polisi waliotaka kuzuia mkutano wao.

Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, Paul Kihwelo alisema aliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kwamba kifungo cha miaka 15 kingemtosha mshtakiwa.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )