Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Sunday, July 1, 2018

Mizengo Pinda Akubali Kuwa Mlezi Wa TACIP......Asema sanaa inaweza kutumika kuondoa umaskini

WAZIRI MKUU mstaafu Mizengo Pinda amesema tasnia ya sanaa ina nafasi kubwa ya kuweza kuondoa umaskini katika ngazi zote kama itatumiwa vizuri.

Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Nzinje, nje kidogo ya Jiji la Dodoma, wakati alipokutana na wawakilishi wa Mradi wa Utambuzi wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP) waliokwenda kumuomba awe mlezi (champion) wa mradi huo.

“Tasnia ya sanaa ni nafasi kubwa ya ajabu ya kuondoa umaskini katika ngazi zote kama tutaitumia vizuri. Nimepokea heshima hii ya kuwa mlezi wa TACIP na naahidi kuwa sitawaangusha,” alisema.

Alisema wiki iliyopita, alipata bahati ya kukutana na viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) jijini Dodoma na alichobaini ni kwamba katika kila eneo walilojadili, walikuwa wakihusisha na suala la sanaa na utamaduni na jinsi inavyoweza kutumika kama njia ya kutoa suluhisho ya tatizo liliopo.

“Wenzetu wako makini sana na kutunza utamaduni wao, lolote atakalojadili lazima aweke umuhimu wa sanaa na utamaduni wao. Wenzetu wameona utamduni ni zana ya kutatua tatizo lolote linaloizunguka jamii yao,” alisema.

“Kwa mfano, katika kukabiliana na tatizo la mazingira, wametumia wasanii kupeleka ujumbe wa kuelezea maovu dhidi ya mazingira na mambo mazuri yanayodumisha mazingira. Katika elimu wametumia sanaa. Kwangu mimi natamani tubaini ni mambo gani tunaweza kujifunza kutoka kwa Wachina katika kukuza sanaa,” alisema.

Alisema kwa Tanzania hali ni tofauti kwa sababu wasanii bado wanatumika kwa ajili ya kutoa burudani tu. “Huku kwetu wasanii wanatumika kutoa burudani, inabidi tubadilishe mtazamo huu kwa kushirikiana na Serikali kupeleka ujumbe huu mpya,” alisema.

Alikiri kuwa tasnia ya sanaa ina washiriki zaidi ya milioni sita ambao hawajawahi kuunganishwa na chombo maalum na kwamba kuanzishwa kwa TACIP kutaleta ukombozi kwenye sekta hiyo muhimu kwa Taifa.

Mapema, Mratibu wa mradi huo, Bw. Macmillan George alimweleza Mhe. Pinda kwamba mradi umepangwa kutekelezwa kwenye kanda sita ambazo ni Pwani Mashariki, Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini na Magharibi. Nyingine ni kanda ya Kati na kanda ya Ziwa.

Alisema wiki ijayo wanatarajia kuanza kukusanya taarifa za wasanii wa sanaa za ufundi kwa kuanza na mkoa wa Dar es Salaam. Wasanii hao wanajumuisha wachoraji, wachongaji (sculptors), wanasanaa za mikono (crafts), wanasanaa jumuishi (peripheral artists), wafinyanzi (ceramics) na wabunifu (designers).

Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nicholaus William ambaye aliambatana na viongozi hao, alisema Serikali inaubeba mradi huo kwa uzito mkubwa.

Alisema kuwepo kwa mradi huo kunatarajiwa kutatua changamoto za wasanii nchini ambazo zimedumu kwa muda mrefu. Kaulimbiu ya mradi huo ni: “Jitambue, Tambulika, Inalipa.”

Mradi wa TACIP (Tanzania Arts and Crafts Identification Project) ambao unatekelezwa kwa ubia kati ya Tanzania Arts and Crafts Identification Project (TAFCA) na DataVision International umelenga kuiwezesha sekta ya sanaa za ufundi Tanzania Bara kuwaongezea kipato washiriki wake, hususan katika kujikwamua kutoka kwenye balaa la umasikini na kuwawezesha kuchangia pato la Taifa.

Mradi huo pia umelenga kuwatambua washiriki wa sekta hiyo na kuwapatia vitambulisho vya kisasa vya kieletroniki; kuanzisha tovuti maalumu ya wasanii hao yenye taarifa za majina, jinsi, umri, mahali walipo na wanachozalisha; kufungua tovuti ya e-commerce portal ili kuwezesha biashara mtandao ya kazi za sanaa za ufundi; kuwahamasisha wajisajili kisheria na kujiunga katika vikundi na vyama ili wawe na nguvu ya sauti na waweze kukubalika kukopa katika taasisi za fedha.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )