Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Friday, September 7, 2018

Akidi ya wabunge yakwamisha upigaji kura ya uamuzi

Kutotimia kwa akidi ya wabunge katika kikao cha nne cha Bunge la 12  leo Ijumaa Septemba 7, 2018 kimekwamisha kufanyika kura ya uamuzi ya kuupitisha au kuukataa  muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali  namba mbili wa mwaka 2018.

Kabla ya Bunge kukaa kama kamati ya Bunge zima, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee aliomba kuhusu utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya uendeshaji wa chombo hicho cha Dola , akieleza kuwa idadi ya wabunge bungeni haifiki nusu ya idadi ya wabunge wote.

Amesema wabunge wote ni 393 lakini waliopo bungeni mpaka muda huo wa mchana leo walikuwa 67, kubainisha kuwa idadi yao hiyo ni ndogo na hawawezi kufanya uamuzi kuhusu muswada huo.

Akijibu kuhusu utaratibu huo, mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amesema watakapofika wakati wa kufanya uamuzi, watazingatia idadi ya wabunge waliopo bungeni.

Hata hivyo, baada ya Kamati ya Bunge zima kumaliza shughuli yake ya kupitia kifungu hadi kifungu, bado idadi  ya wabunge bungeni ilikuwa ndogo na kumfanya Halima kunyanyuka tena, kukumbushia jambo hilo.

“Mheshimiwa mwenyekiti utoe maelekezo kengele ipigwe walioko nje waje, kwa makatibu wahesabu wabunge walioko bungeni halafu utaratibu wa kikanuni ufuatwe,”amesema Mdee.

Wakati Halima akieleza hayo naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, ameshauri kuwakata posho wabunge ambao hawakuwepo bungeni kwa wakati huo isipokuwa waliokwenda msikitini na wale wenye ruhusa.

“Mwenyekiti ukiwatoa wale walioenda msikitini na wale walioomba ruhusa kuna wale wazembe wa kutohudhuria Bunge. Ninashauri wakatwe posho ya siku ya leo,” amesema Manyanya.

Katika ufafanuzi wake Najma amesema, “natoa dakika tatu kengele ipigwe ili waingie waliokuwepo nje.”

Licha ya tangazo hilo idadi ya wabunge bado haikutimia na hivyo kuamua kuahirisha Bunge hadi Septemba 10, 2018 saa 3:00 asubuhi.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )