Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Monday, September 10, 2018

Rais Magufuli Amgomea Waziri Wake Hadharani

Rais  Magufuli amekataa ombi la Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu la kutaka jimbo lake liwe halmashauri.

Rais Dk.Magufuli alisema kuanzisha maeneo mapya ya utawala kumekuwa kukiongeza gharama za uendeshaji.

Alisema ni bora fedha hizo akazitumia kuwaletea wananchi maenedeleo kuliko kuongeza halmashauri.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mji wa Mwandoya wilayani Meatu aliposimama kusalimia wananchi, wakati wa ziara ya kukagua shughuli za maendeleo.

Awali Mpina alimwomba Rais Dk. Magufuli kuwapatia halmashauri wananchi wa Kisesa kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kiutawala.

“Wananchi wa Kisesa wamekuwa wakipata wakati mgumu kwenda mji wa Mwanhunzi  ambapo kuna ofisi za halmashuari.

“Wilaya ya Meatu kuna majimbo mawili na yote yanategemea halmashauri moja. Hawa wananchi mheshimiwa Rais, wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya 100 kwenda makao makuu ya mkoa, kilomita 60 kwenda makao makuu ya halmashauri.

“Mheshimiwa Rais umbali huo wote ni mrefu, sisi hatuombi wilaya, tunaomba utupatie halmashauri ya kwetu sisi wenyewe,” alisema waziri huyo.

Mpina alisema uwezo wa kujiendesha kama halmashauri upo, kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu zaidi ya 170,000.

Alisema mbali na idadi ya watu, Jimbo la Kisesa lina uwezo wa mapato, kwani limekuwa likikusanya zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka pamoja na kuwapo kwa miundombinu mingine ya kutosha kuwa halmashauri.

Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wananchi, Waziri Mpina alisema kupatikana kwa halmashauri kutasababisha wananchi wa jimbo hilo kupata maendeleo kwa haraka.

Akizungumzia ombi hilo, Rais Magufuli alisema kwa sasa hawezi kuanzisha maeneo mapya wakati wananchi wengi bado ni maskini na badala yake atahakikisha anawaletea maendeleo na si kuwaletea halmashauri.

Rais Magufuli alilazimika kutoa mifano mbalimbali ya majimbo yenye maeneo makubwa, lakini kuna halmashauri moja, ambapo alitolea mfano wa halmashauri ya Chato ambayo alieleza kuwa idadi ya watu ni zaidi ya 400,000.

“Kuna majimbo mengi tena makubwa zaidi ya hili na yana idadi kubwa ya watu kuliko hapa Kisesa, kuna halmashauri moja, siwezi kuleta halmashauri wakati najua itaongeza gharama za uendeshaji,” alisema Rais Magufuli.

“Kupanga ni kuchagua, niache nishughulikie masuala ya barabara, umeme, maji na afya, siyo kuwaletea halmashauri, haya maombi yenu yatakuwa baadaye lakini siyo sasa hivi, siwezi kuleta halmashauri, nitaleta maendeleo,”alisema Rais Maguli.

Alisema hawezi kuwadanganya kuwa atawapatia  halmashauri wakati jambo hilo hawezi kulifanya kwa sasa.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )