Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, October 6, 2018

Jeshi La Polisi Mwanza Lanasa Mtandao Wa Majambazi Sugu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza  limemkamata Jambazi mmoja sugu aitwaye Peter Thomas  Nyanchiwa  kwa kosa la wizi wa gari lenye namba T.122 DLY aina ya Toyota Costa mali ya Ismail Abdallah na kukamata silaha bastola aina ya Berete  yenye namba H44780Y, ikiwa na risasi kumi na mbili ndani ya magazini huko maeneo ya Runzewe Mkoani Geita.


Tukio hilo limetokea wiki moja iliyopita, hii ni baada ya mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa na wenzake wawili kukodisha gari hilo toka kwa mmiliki wa gari aliyop hapa jiji Mwanza kwa ajili ya kwenda kuwachukua watalii waliokuwa wameharibikiwa gari awapeleke mbugani kuendelea na utalii katika mbuga ya wanyama ya Serengeti.

Lakini walipofika Serengeti eneo la Nata  mtuhumiwa akishirikiana na wenzake wawili walimshusha dereva kwenye gari na kumpiga risasi kwenye maeneo ya taya kisha waliondoka na gari wakiamini kuwa  tayari amefariki dunia. Wananchi waishio jirani  na eneo hilo baada ya kusikia mlio wa risasi walikwenda eneo la tukio kutoa msaada  na kumkimbiza dereva huyo hospitali ya Wilaya ya Serengeti kisha walitoa taarifa Polisi.

Majambazi hao baada ya kutenda uhalifu huo waliondoka  na gari hilo kurudi walipotoka wakipitia barabara ya bariadi, Shinyanga, Kahama ambapo wamedai kuwa walikuwa wakielekea Nchini Uganda kwenda kuliuza. Wakati wakiendelea na harakati hizo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tulipata taarifa hizo na kwa kutumia kikosi chetu kabambe  na chenye uweledi wa hali ya juu na kushirikiana na wenzetu wa Mkoa wa Mara na Geita tulianza ufuatiliaji wa kina ambapo vijana wetu walifanikiwa kufukuza gari hilo maeneo ya Runzewe

Mkoani Geita waliliamuru kusimama lakini majambazi hao walianza kuwarushia risasi askari wetu .Lakini kutokana na umahiri wa askari  waliendelea kukabiliana na majambazi hao na baada ya majambazi hao kuzidiwa watuhumiwa wawili walifanikiwa kutoka kwenye gari na kutokomea porini na momja wao alikamatwa akiwa na silaha aina ya bastola (pistol) na risasi kumi na mbili. Pia upekuzi wa kina ulifanyika ndani ya gari hiyo yenye usajili namba T.122 DLY aina ya Toyota Costa ambapo tulikuta vitu vifuatavyo;
 1.     Gari iliyoibiwa namba  T.122 DLY aina ya Toyota Costa.
 2.     Magazini mbili za silaha aina ya AK 47, moja ikiwa na risasi 30 na nyingine ikiwa haina risasi.
 3.     Bastola aina ya Berete namba H44780Y
 4.     Leseni/kitabu cha bastola chenye namba 00097399
 5.     Passport namba AB362201 ya Peter Thomas Nyanchiwa.
 6.     Hati ya dharura ya kusafiria ya namba AB10528412 ya Rashidi Rashidi
 7.     Cheti cha Veta namba 35912 cha Abdallah Omary Shabani
 8.     Plate namba mbili nyeupe ya gari namba T.876 DMB aina ya Toyota Costa.
 9.     Kivuli cha kadi ya gari namba 6032015 ya gari namba T.876 DMB Toyota costa
 10.     Simu tecno mbili, simu fero moja na simu Samsung moja
 11.     Line za simu nane.
 12.     ATM Card tatu, moja ya CRDB na mbili za NMB
 13.     Vifaa vya kuvunjia -plaizi 1, pipe range 1, nyundo 1 na spanner 1.
 14.     Driving licence ya Peter Thomas.
 15.     Fedha kiasi cha TSH 1,330,000/=, za kusafishia njia
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea na upelelezi pamoja na mahojiano na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. Aidha msako mkali wa kuwatafuta wenzake waliotoroka bado unaendelea. Dereva aliyejeruhiwa kwa risasi anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya vijana wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na uhalifu tukiwataka waache kwani ni kosa la jinai, lakini pia wanaweza kujihatarishia maisha yao hivyo wafanye kazi zilizo halali za kujipatia kipato. Sambamba na hilo tunawasisitiza wananchi waendelee kutupa ushirikiano Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ili tuendelee kuimarisha amani katika Mkoa wetu.

Katika tukio la Pili; Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tumemkamata Mtu mmoja tapeli anayefahamika kwa jina la Nkwabi Samweli @ Kabinza, miaka 26, Mkazi wa Mtaa wa Pasiansi kwa kosa la kijifanya tabibu (daktari) wakati si daktari katika hospitali ya rufaa ya Bugando, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo limetokea tarehe 3/10/2018 majira ya saa 01:00hrs mchana, mara baada ya uongozi wa hospitali hiyo kupokea malalamiko toka kwa wagonjwa ya kuibiwa mara kwa mara wodini. Ndipo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana  na uongozi wa hospitali ya rufaa ya Bugando tuliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa chumba cha upasuaji na akiwa amevalia sare kama ambazo huvaliwa na madaktari  wakiwa chumba cha upasuaji (thieta).

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa ili kujua alipopata sare hizo na jinsi alivyoingia katika chumba hicho cha upasuaji pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kujifanya watumishi wa serikali wakati sio waache kwani ni kosa kisheria na endapo mtu atabainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Aidha na wale wote ambao waliwahi kuchukuliwa fedha wafike kituoni ili kumtambua kwani tapeli huyu anachafua jina la hospitali yetu ya rufaa ya Bugando.

Katika tukio la Tatu; mtoto wa kike aliyefahamika kwa jina la Solile Emmanuel, miaka 5, amefariki dunia katika  ajali ya moto iliyounguza nyumba yao ya chumba kimoja na sebule iliyojengwa kwa tofali za tope na kuezekwa kwa bati na kuteketeza mali na vitu vyote vilivyomo ndani ya nyumba hiyo huko mtaa wa Nh’obola Wilayani Nyamagana.

Tukio hilo limetokea tarehe 03/10/2018 majira ya saa 17:00 jioni, wakati marehemu alipoachwa peke yake chumbani akila chakula huku wazazi wake wakiwa bustanini wakilima. Inadaiwa marehemu alikuwa akichezea njiti ya kiberiti na kupelekea kuwasha moto ulioanza kuunguza godoro, nguo na hatimaye kushika nyumba nzima hali iliyopelekea marehemu kukosa hewa  na baadae kufariki dunia.

Polisi tulifika kwa haraka eneo la tukio na kushirkiana na wananchi kutoa msaada lakini moto ulikuwa tayari umepoteza uhai wa mtoto na kutekeza mali na vitu vyote katika nyumba hiiyo. Thamani ya mali na vitu vilivyoteketea katika ajali hiyo bado haijafahamika. Mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunawataka na kuwasisitiza wazazi na walezi kuwa waangalifu na watoto wakati wote, waache tabia ya kuwaacha watoto kwenye nyumba peke yao kwani kunaweza kuhatarisha usalama wao na baadae kupata majeruhi au kufariki dunia.

Katika tukio la nne; Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia kijana mmoja mwizi/Jambazi  anayefahamika kwa jina la Jackson Elias @ Longoko, miaka 20, mkazi wa mtaa wa Shamaliwa Igoma, kwa kosa la kuvunja nyumba yenye mashine ya kusaga usiku na kuiba mota tatu katika kijiji cha Lugeye Wilayani Magu, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo limetokea tarehe 28/09/2018 majira ya saa 23:00hrs usiku, ambapo mtuhumiwa tajwa hapo juu akishirkiana na wenzake watatu walivunja nyumba hiyo usiku na kuiba moto tatu. Wananchi walitoa taarifa polisi ambapo tulifanya ufuatiliaji wa haraka na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu na tayari wamefikishwa mahakamani wakiwa na mota tatu walizoziiba, huku mtuhumiwa tajwa hapo juu akifanikiwa kutoroka.

Polisi tuliendelea na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa aliyetoroka, ndipo tarehe 03/10/2018 majira ya saa 11:00hrs asubuhi katika mtaa wa Shamaliwa Igoma tulifanikiwa kumkata mtuhumiwa akiwa nyumbani kwake. Polisi tulifanya upekuzi hapo nyumbani kwake na kufanikiwa kukamata vitu vifuatavyo;
 1.     Bendera moja ya Taifa.
 2.     Mkasi mmoja mkubwa wa kukata vyuma na mabati.
 3.     Bisibisi moja
 4.     Nondo moja iliyochongwa
 5.     Plaizi moja
 6.     Tindo moja ya kufungulia kufuli.
Polisi tunaendelea na mahojiano na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo na kuendelea kusisitiza wananchi wenye tabia ya kiuhalifu kuacha mara moja kwani Mkoa wa Mwanza si mahali pake hivyo waache  na wajihusishe na shughuli halali za kuwaingizia kipato. Pia tunawataka wananchi waache kumiliki nyara za serikali kwani ni kosa  kisheria na atakae bainika atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Katika tukio la tano; watu wawili  wanashikiwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kujifanya watumishi wa serikali kisha kuwatapeli wananchi wawili feedha kiasi cha laki moja na elfu sitini (TSH 160,000) huku wakiendelea kudai kiasi cha milioni moja ( TSH 1,000,000) ili wawapatie nafasi watoto wao ya kwenda kwenye mafunzo ya Uaskari katika chuo cha taaluma ya Polisi Moshi (CCP) na mwingine mtoto wake aweze kwenda kwenye chuo cha udaktari  cha Haidom kilichopo Mkoani Manyara , kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo limetokea tarehe 03/10/2018 majira ya saa 13:30hrs mchana, katika mtaa wa Nyegezi stand, hii ni baada ya polisi kupata taarifa toka kwa raia wema kwamba katika mtaa tajwa hapo juu wapo watu wanaowatapeli wananchi kwa kujifanya watumishi wa serikali. Polisi tulifanya ufuatiliaji katika eneo hilo  na kuweka mtego na baadae tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili.

Watuhumiwa waliokamatwa ni 1.Elias Malelemba @ Mayombya, miaka 47, fundi ujenzi, Mkazi wa Dar es Salaam na 2.. Sharifu Hamis @ Mgene, miaka 58, Mkazi wa Mkarama Mkoani  Singida. Polisi tunaendelea na upelelezi pamoja na mahojiano na watumiwa wote, pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa watu wanaodhani kuwa Mwanza ni sehemu ya kufanya uhalifu kuwa waache kwani tutawakamata na kuwashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Imetolewa na;
Jonathan Shanna – ACP.
Kamanda wa Polisi (M) Mwannza.
06 October, 2018.

Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )