Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Sunday, October 7, 2018

Salute Yamponza Afisa Magereza Mbele ya Waziri Kangi Lugola

Heshima  ya saluti ambayo askari wamekuwa wakiwapigia viongozi au wakuu wao kama ishara ya utii na heshima, imemponza ofisa wa Magereza mkoani Mbeya.

Tukio hilo lilitokea juzi wakati Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alipofanya ziara yake ya kikazi kwenye Gereza la Luanda, mkoani Mbeya.

Kwenye ujumbe wa video uliosambaa kwenye mitandao mbalimbali, Lugola anaonekana akiwasili kwenye gereza hilo na kupigiwa saluti na viongozi mbalimbali wa gereza hilo.

Viongozi hao wanaonekana wakimpigia saluti Waziri Lugola huku wakiwa wameweka fimbo zao kwapani kama ilivyo kawaida kwa maofisa wa majeshi ya ulinzi na usalama wanapopiga saluti.

Ilipofika zamu ya askari mmoja ambaye jina lake halijafahamika, alipiga saluti akiwa hana fimbo hiyo hali ambayo ilimshtua Waziri na kuhoji kwa nini hana fimbo kama wenzake.

"Hivi unaruhusiwa kupiga saluti kama huna fimbo? Nakuuliza unaruhusiwa kupiga saluti bila fimbo kama wenzako? Hilo ndilo swali langu," alihoji Lugola kwa ukali.

Waziri Lugola alihoji kama askari huyo anafahamu kuwa haruhusiwi kupiga saluti bila kuwa na fimbo hiyo na kama anajua ni kwa nini ameamua kufanya ubangaizaji.

"Kama hujui ulitakiwa ukae huko usiwepo hapa kwa sababu hujakamilika. Lazima tufundishane nidhamu," alisema Waziri Lugola huku sauti za viongozi zikisikika kumuombea msamaha ofisa huyo.

Ofisa huyo alikiri kuwa amefanya makosa kwa kutokuwa na fimbo hiyo kama wenzake na kuomba msamaha ndipo Waziri Lugola alipomwamuru kwenda kutafuta fimbo hiyo na kurudi kabla hajaondoka.

"Nenda ulete hiyo fimbo uje nayo ndipo unipigie saluti maana hii uliyonipigia haina tofauti na kughushi. Hii saluti umeighushi usifanye, hivyo rekebisha kuwa na heshima. Nenda kalete fimbo haraka kabla sijatoka hapa," aliagiza Lugola na askari huyo alitii amri hiyo na kuondoka haraka eneo hilo.

Kiongozi wa askari hao alipotaka kumtetea, Waziri Lugola alisema hakuna utetezi hapo kwa sababu hata kama angekuwa wapi, haruhusiwi kupiga saluti bila kukamilika.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )