Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Wednesday, November 21, 2018

Kampuni ya Reginald Mengi Kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari Hapa nchini

Kampuni ya IPP Automobile Ltd imeingia ubia na Kampuni ya Youngsan ya Korea kusini kuwekeza katika sekta ya usafirishaji na uchukuzi kwa kuwa na kiwanda cha kuunganisha magari nchini.
 
Gari la mwanzo kutoka katika uwekezaji huo wa zaidi ya bilioni 22, litaingia sokoni kati ya Septemba na Oktoba mwaka 2019.
 
Kiwanda hicho kinachotarajiwa kuunganisha magari 1000 kwa mwaka kitatoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi 500, idadi inayotarajiwa kuongezeka kadri ya muda unavyokwenda.
 
Kiwanda hicho kitajengwa eneo la Kurasini, ujenzi utaanza mwanzoni mwa mwaka ujao.
 
Makubaliano ya uanzishwaji wa kiwanda hicho yalitiwa saini jijini Dar es Salaam jana kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi na Bw Thomas Choi Mkurugenzi na Mwakilishi wa Kampuni ya Youngsan Glonet ya Korea ambao ndio wawakilishi wa kiufundi wa kampuni ya Zyle Daewoo Commercial Vehicle na Hyundai Motor Corporation ya Korea Kusini huku tukio hilo likishuhudiwa na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Song Geum-young .
 
Katika mazungumzo wawakilishi hao na balozi walisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho, kumelenga kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini.
 
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti Mtendaji  wa IPP,Dk. Reginald Mengi alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho, ilikuwa moja ya ndoto zake kama hatua ya kuitikia mwito wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, inayosisitiza kasi ya ujenzi wa viwanda nchini.
 
“Hakuna kinachoshindikana ukiwa na nia, hata Rais wetu anapambana katika mambo ambayo wengi waliona yanashindikana, amenunua ndege na  kufanya mengine mengi..hii ni hatua kubwa katika kukuza maendeleo yetu,” alisema Dk. Mengi.
 
Alisema kiwanda hicho kikianza kazi, kitatoa ajira kwa Watanzania, pia kitasaidia kuongeza mzunguko wa biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kuiingizia mapato serikali kupitia kodi mbalimbali.
 
Aidha, alisema mipango yake ya baadaye ni kuhakikisha wanajenga kiwanda chenye uwezo wa kutengeneza magari kuanzia mwanzo hadi inapokamilika kutoka katika hatua hiyo ya uunganishaji, jambo alilosema litazidi kuitangaza Tanzania.
 
Magari yanayotarajiwa kuunganishwa kupitia kiwanda hicho ni mabasi, malori na magari madogo, ambapo kwa mujibu wa Balozi wa Jamhuri ya Korea, Mh. Song Geum-young magari hayo ni ya kisasa.
 
Alisema Jamhuri ya Korea imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa magari na kwamba anaamini kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho nchini, kutasaidia kuleta mapinduzi katika sekta ya viwanda na kuleta tija kimaendeleo na amewahakikishia Watanzania kuwa Korea ni wajuzi wa kutengeneza magari yenye viwango vya juu vya ubora duniani.
 
Magari yatakayotoka katika kiwanda hicho ni ya biashara ya tani 2.5; 3.6 na malori  ya tani 18 hadi 28; mabasi ya mita saba,9 na 12 na magari ya kujinafasi  (SUV) na magari madogo mengine.
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

taboola apo chini
....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )