Pakua App Yetu Playstore
<< BOFYA HAPA>> Kui Install

Saturday, December 8, 2018

Waziri Wa Kilimo: Korosho Zote Zitabanguliwa Nchini

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo- Mtwara
Serikali imeagiza korosho zote inazonunua kwa wakulima kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko kuanza kubanguliwa nchini.

Agizo hilo la serikali limetolewa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 8 Disemba 2018 wakati akizungumza kwenye Mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho kwenye ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Hasunga alisema kuwa Mkakati wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Pombe Magufuli ni kuwanufaisha wakulima nchini hivyo maamuzi ya kununua korosho ni sehemu ya maamuzi mema kwa manufaa ya wakulima wote.

Alisema wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima mpaka hivi sasa tayari wakulima 77,380 wamekwishalipwa hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalumu badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.

Mhe Hasunga aliongeza kuwa Korosho zitakazoruhusiwa kwenda nje ya nchi ni zile Tani 2000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.

“Hakuna kampuni yoyote wala mfanyabiashara yoyote anayeruhusiwa kusafirisha korosho nje ya nchi baada ya tamko la serikali kutolewa” Alikaririwa Mhe Hasunga

Aliongeza kuwa kutokana na uamuzi huo wa serikali imechukua takwimu zote za korosho zilizozalishwa mwaka jana ambazo zilikuwa bado hazijabanguliwa hivyo haitegemei kusikia wafanyabiashara wakisema wana korosho nyingi walizohifadhi badala yake kuwa wazalendo kwa kusema ukweli.

“Tuwe na uwezo wa kubangua ama hakuna lakini korosho zote zitabanguliwa nchini, hivyo wito wangu kwa wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya ubanguaji usiku na mchana” Alisema

Mhe Hasunga aliongeza kuwa serikali imeanza mchakato wa kuwafuatilia baadhi ya wafanyabiashara wenye uwezo wa kujenga viwanda kwa kufunga mitambo ndani ya muda mfupi.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Joseph Kakunda (Mb) amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda hivyo Serikali haitakubali kuhujumiwa inapoendelea kuboresha uwekezaji, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na upendo hivyo wafanyabiashara kote Duniani wana wajibu wa kujitokeza na kuanzisha biashara zao pasina kadhia yoyote.

Aliongeza kuwa mawakala wanaotumiwa kuvuruga uchumi wa viwanda na serikali kwa ujumla wake watachukuliwa hatua zinazopaswa kwa mujibu wa sheria.

MWISHO
Advertisement
==


Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Loading...
==

....

===
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )