Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Wednesday, January 9, 2019

Ufafanuzi Toka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kuhusu Usimamizi Kwa Watoa Huduma Ndogo Za Fedha

adv1
Benki Kuu ya Tanzania imetoa tangazo kwa umma kupitia tovuti yake (www.bot.go.tz) likiwataka watu na taasisi zote zinazofanya biashara ya huduma ndogo za fedha zilizoko Tanzania Bara (isipokuwa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo – SACCOS) kutoa taarifa zitakazotumika katika utayarishaji wa Kanuni za Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha. Taarifa hizo zinatakiwa kutumwa Benki Kuu ya Tanzania hadi tarehe 31 Januari 2019.

Benki Kuu inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusu tangazo hilo:

Lengo la tangazo hilo siyo kuvifunga au kuvibana vikundi vya kijamii kama VICOBA, watu binafsi na taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kama ambavyo inapotoshwa na baadhi ya watu na mitandao mbalimbali ya kijamii, bali ni kukusanya taarifa za awali kuhusu huduma hizo. 

Kama ilivyoainishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupitisha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, lengo la sheria hiyo  ni kuwalinda wadau wote wanaohusika na huduma hizi (watoaji na watumiaji) kwa kuziwekea utaratibu mzuri zaidi wa uwekaji kumbukumbu, uendeshaji na uongozi kwa ujumla. 

Pia kuwalinda wamiliki na watumiaji wa huduma hizi dhidi ya vitendo vinavyoweza kupelekea kupoteza fedha na mali zao, pamoja na kuzuia watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutumika kufanya uhalifu ikiwemo utakasishaji fedha haramu.
 
Benki Kuu inafahamu kuwa baadhi ya watu binafsi, taasisi na vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VICOBA, havina usajili rasmi na hivyo havitambuliki kisheria. 

Kwa kutambua hilo, Sheria imeweka kipindi cha mpito cha mwaka mmoja (kuanzia sheria itakapoanza kutumika rasmi) kwa wote wanaojihusisha na utoaji huduma ndogo za fedha, kujipanga ili wawe tayari kusimamiwa pale kanuni zitakapokuwa zimetolewa rasmi. 

Hivyo, katika kipindi hiki cha mpito, siyo kosa kwa watu binafsi, taasisi na vikundi vya kijamii kutokuwa na usajili rasmi.  

Aidha, Wadau wote watashirikishwa kikamilifu katika utayarishaji wa Kanuni hizo, na mara zitakapokuwa tayari na kutolewa na Benki Kuu ya Tanzania, maelezo zaidi kuhusu usajili yatatolewa.

Benki Kuu inawasihi wananchi wote kutokuwa na taharuki na inasisitiza kwamba uamuzi wa kusimamia watoa huduma ndogo za fedha umechukuliwa kwa nia njema na  kwa faida ya watumiaji na watoaji wa huduma hizi.

Aidha, Benki Kuu  inautahadharisha umma kujiepusha na taarifa na miongozo inayotolewa kiholela na watu, kampuni na mashirika ambayo yanajitangaza kufanya shughuli za uandikishaji wa watoa huduma ndogo za fedha kwa wananchi kwa niaba ya Serikali au Benki Kuu. 

Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu, kampuni au shirika lolote litakalojihusisha na vitendo vya kuwakanganya wananchi kwa lengo la kupotosha au/na kujipatia mapato haramu.

Tunawahamasisha wananchi kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tangazo hili zinazoendelea kutolewa na Benki Kuu katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha Tanzania Bara.

Kwa ufafanuzi/maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu   022-2235585/0767503145 au barua pepe:vctarimu@bot.go.tz, nfmongateko@bot.go.tz, dasasya@bot.go.tz, botcommunications@bot.go.tz, au tembelea Benki Kuu Makao Makuu Mtaa wa 2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )