Je, Unatafuta Kazi au Ajira?
<< BOFYA HAPA>> Kupata Ajira Yako Leo

Tuesday, February 19, 2019

Nape Nnauye Asimulia Machungu ya Bunge Kutooneshwa LIVE

adv1
Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye, amesema anatambua maumivu wanayoyapata wananchi kutokana na Bunge kutokuoneshwa mubashara (live).

Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama (CCM), alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha 360 kilichorushwa na Clouds Tv jana.

Alisema anajua kuwa wananchi wanaona jambo hilo halikuwatendea haki, lakini ni kutokana na kuwa mchakato haukukamilika ipasavyo.

Nape alisema utungaji wa kanuni za kusimamia na kuendesha studio za Bunge haukushirikisha wadau ndiyo sababu ya Bunge kutokurushwa mubashara.

“Hata ushiriki wa wananchi katika shughuli za Bunge umepungua sana kwa kuwa wanaona vipindi vichache tu, hivyo tungetengeneza kanuni ambazo zitasaidia watu wote kuona zingesaidia kurejesha hali kawaida,” alisema Nape.

Alisema hata hivyo sheria za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), haziruhusu kuweka matangazo ya biashara wakati wa kuonesha vipindi vya Bunge jambo ambalo linaviumiza vituo vya televisheni na kushindwa kumudu kurusha mubashara.

“Kama Bunge ni la umma, linaendeshwa na fedha zetu za walipakodi, turuhusu kuweka matangazo katikati, lakini turuhusiwe kurusha ‘live’, jambo hili ni la kukaa mezani na kujadili tu,” alisema Nape.

Alisema wakati anachaguliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, Michezo na Wasanii alikuta uongozi wa Bunge walikubaliana kuanzishwa kwa studio hiyo na tayari walikuwa wametenga fedha kuianzisha.

“Nilikuta TV pekee inayorusha Bunge ilikuwa ni TBC ambayo ilikuwa haitengewi fedha kwa shughuli hiyo, huku ikitumia Sh bilioni nne kwa mwaka kufanya kazi hiyo,” alisema Nape.

Alisema aliamua kuiondoa TBC kurusha matangazo hayo na kama Bunge lingehitaji kufanya kazi hiyo wangetakiwa kuilipa gharama inazotumia.

“Serikali ya awamu ya tano ilikuja na mkakati wa kupunguza matumizi na kila waziri alitakiwa kuangalia eneo lake, nami nikaona hapa tunaweza kupunguza matumizi,” alisema Nape.

Aliongeza kuwa hata hivyo Bunge tayari lilikuwa limeanza ujenzi wa studio zake kama ilivyo kwa nchi za Jumuiya ya Madola ambao hutumia utaratibu huo kulinda heshima za Bunge.

“Bunge liliamua kuviondoa vituo vingine vya televisheni ili waweze kuchukua taarifa kutoka studio za Bunge, lakini mzigo wote nilibebeshwa mimi kama waziri.

“Kama ‘screen’ zote bungeni zinaonesha kila kinachoendelea, kinachokosekana ni namna ya kwenda kuzichukua taarifa hizo na kuzirusha japo kwa kuchelewa dakika kadhaa ili mradi ziwafikie wananchi,” alisema Nape. 

Nape pia alizungumzia sakata la kutishiwa kupigwa kwa bastola na anayedaiwa kuwa ni askari polisi, wakati akitaka kuzungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya uteuzi wake katika nafasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutenguliwa.

Alidai anamfahamu aliyemtishia kumpiga kwa bastola, waliomtuma na waliosuka mpango huo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliokuwa ufanyike hotelini, lakini ukafanyika kando ya barabara Machi 23, 2017.

"Hatua kubwa niliyochukua baada ya kutishiwa kwa bastola niliamua kusamehe. Mimi nimelelewa na mcha Mungu na unapofanyiwa jambo la kuumiza sana moyo wako, njia sahihi ni kusamehe," Nape alisema.

Alisema aliwasamehe wote waliohusika na utaratibu mzima na alipokea ushauri wa wanasheria waliomtaka kufungua kesi kwa kuwa alikuwa na nafasi kubwa serikalini, ili kuwa funzo kwa wenye kufanya vitendo kama hivyo, lakini hakuona kama ingekuwa na matokeo mazuri.

Alisema hawezi kuwataja waliohusika, lakini si watu wa mtaani na hakuripoti tukio hilo kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni wakati huo, Suzan Kaganda, alikuwapo eneo la tukio.

"Niliamua kuwasamehe wote kwa sababu sikuona kama itakuwa na matokeo mazuri na sikuripoti polisi kwa sababu walikuwapo eneo la tukio, nikaona sasa hapa nitamshtaki nani kwa nani, kwa sababu RPC alikuwapo na polisi wengi waliovaa sare na waliovalia kiraia walilishuhudia tukio zima," Nape alisema.

Alisema haamini kama aliyemtishia kumpiga kwa bastola alikuwa na nia ya dhati ya kumpiga, bali alipaniki kulingana na mazingira ya tukio lile.

Nape alisema alibisha kutofanya mkutano kama alivyotakiwa na mtu huyo kwa sababu alikatazwa kwa amri na si kwa hoja ilhali anazifahamu haki zake na sheria za nchi.

“Walikuja kwa lengo la kunivurugia mkutano, nikasema sawa, tukatoka nje kwa ajili ya kufanya mkutano, lakini akaja kijana, hajavaa sare, akaniambia nisifanye mkutano niingine kwenye gari, sijamtambua ni nani, nikamwambia hapana, 'we(we) ni nani na kwanini unanizuia?' Nikaonekana nakaidi amri ambayo ni ujinga," Nape alisema.

Nape alisema asilimia 99 ya watu aliozungumza nao baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais John Magufuli, walimshauri asifanye mkutano na waandishi wa habari.

Alisema alifanya uamuzi wa mwisho baada ya kupokea ushauri huo kwa kuwa lilikuwa ni jambo kubwa lililotaka kufungwa kwa mjadala wake ambao baadaye ungemuumiza zaidi.

"Lile jambo lilikuwa ni kubwa na lilikuwa limekamata mioyo ya watu, 'media' (vyombo vya habari) imekamata mioyo ya watu. Sasa usipofunga agenda, mjadala ungekuwa mkubwa na ungeniumiza mimi, ningelazimika kuanza kujieleza. Hivyo, nilifanya vile ili kuokoa taswira ya nchi yangu," alisema.

Alisema kuwa anaamini kuwa, kama mkutano wake na waandishi wa habari ungefanyika salama, ungesaidia kuokoa taswira ya nchi, serikali ingebaki na chama kingebaki salama.

“Nilikuwa nimeandika ninachotaka kusema na 'nikashare' (nikasambaza) na baadhi ya viongozi wa dola waone kama kuna tatizo na wakasema hawaoni tatizo. Nikaruhusiwa niende na nikaenda, nikakuta vyombo vya dola vimetanda," Nape alisema.

Aliendelea kueleza kuwa, watu waliofika kwenye mkutano huo, ni wengi, akibainisha kuwa mbali na waandishi wa habari tu, dada zake ambao hawakuwa na taarifa zake, pia walihudhuria.

Nape alidai kuwa, wakati ananyooshewa silaha, naye alikuwa nayo na mlinzi wake pia alikuwa nayo, hivyo kama wangeamua kuzitumia, amani ingetoweka.
adv
Loading...

Advertisement
Usipitwe na Habari Yoyote. Install Mpekuzi App kwenye Simu Yako Upate Habari Zetu kwa Wepesi Zaidi

==>>... << BOFYA HAPA  Kui Install>>
Mgid
taboola apo chini
hapa
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )